Guterres abainisha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa anatiwa wasiwasi na kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu duniani na akasema mwenendo huo hauvumiliki.
Akizungumza huko Islamabad Pakistan katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa; Shah Mahmood Qureshi Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amesema kuwa leo hii tunashuhudia namna wahajiri au wakimbizi katika baadhi ya nyakati wanavyoshambuliwa na wanasiasa wenye misimamo ya kufurutu ada.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa tunapasa kukabiliana kwa nguvu na vitendo hivyo vya chuki dhidi ya Uislamu.
Antonio Guterres ameongeza kuwa uenezaji wa chuki ni moja ya nyenzo muhimu zaidi katika uwanja huo na Umoja wa Mataifa hivi karibuni umeanzisha mpango kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya uenezaji chuki dhidi ya Uislamu duniani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa pande zote zinapasa kushikamana na kuwa kitu kimoja kikamilifu ili kuweza kukabiliana na aina zote za sera za kichochezi za wanasiasa kupitia uenezaji wa vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na aina nyingine za chuki ili kujipatia kura.
Shah Mahmood Qureshi kwa upande wake ameeleza kutiwa wasiwasi na kuongeza chuki dhidi ya Uislamu na kueleza kuwa mwenendo huo ni hatari sana. Amesema vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vimeathiri pakubwa siasa za Ulaya.
Serikali za Ulaya zinatekeleza sheria kali za kuwabana na kukabiliana na Waislamu katika uhuru wa kuabudu na kutekeleza faradhi zao za kidini na katika suala la mavazi ya Kiislamu kwa wanawake wa dini hiyo.