Russia na Hamas ya Palestina zajadili "Muamala wa Karne"
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) wamekutana mjini Moscow na kujadili matukio ya Palestina.
Katika mkutano huo wa jana Jumatatu mjini Moscow, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) Ismail Hania wamezungumzia mpango wa Marekani uliopewa jina la "Muamala wa Karne."
Aidha makubaliano ya amani baina ya makundi ya kisiasa ya Palestina na uhusiano wa pande mbili baina ya Palestina na Russia zilikuwa katika ajenda kuu za kikao hicho cha jana.
Awali, Hamas ilikuwa imetangaza kuwa, Hania ataenda Moscow kujadili na viongozi wa Russia mikakati na njia za kukabiliana na mpango huo wa Kimarekani ulio dhidi ya Wapalestina.
Kabla ya kwenda Russia, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) alikuwa amezitembelea Qatar na Uturuki.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema afisa huyo wa ngazi za juu wa Hamas anataka kuundwa muungano wa pande tatu wa Russia, Qatar na Uturuki kwa ajili ya kukabiliana na hatua za upande mmoja za Marekani na 'Muamala wa Karne."
Njama hizo za Marekani na Israel dhidi ya Wapalestina kwa jina la 'Muamala wa Karne' zilizozinduliwa Januari 28 mjini Washington, zimelaaniwa na kukosolewa na makundi yote ya kisiasa ya Palestina, nchi za Kiarabu na Kiislamu, asasi za kieneo na kimataifa, Umoja wa Ulaya na nchi nyingi duniani.