Russia: Katika suala la JCPOA Marekani imetengwa kikamilifu
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Russia amesisitiza kwamba nchi zote zina msimamo mmoja dhidi ya Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba Washington imetengwa kikamilifu.
Mikhail Ulyanov, Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna, Austria ameyasema hayo katika mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kwamba nchi nyingi zinaamini kwamba mapatano ya nyuklia ya JCPOA yalikuwa muhimili muhimu wa udiplomasia na msaada mkubwa kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia duniani. Mikhail Ulyanov ameongeza kwa kusema kuwa hivi sasa Marekani imetengwa kikamilifu kuhusiana na suala hilo katika Baraza la magavana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Hivi karibuni serikali ya Marekani iliwasilisha muswada kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikitaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika baraza hilo. Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vikwazo hivyo vinatakiwa kufikia tamati mwezi Oktoba mwaka huu. Kupasishwa muswada huo uliowasilishwa na Marekani kunahitajia kwa uchache uungaji mkono wa wajumbe 9 wa Baraza la Usalama sambamba na kutopigiwa kura ya veto na nchi zenye haki ya kura hiyo kama vile Russia na China. Hii ni katika hali ambayo nchi mbili hizo zimetangaza kwamba zitazuia juhudi zozote za Marekani kutaka kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.