Naibu Katibu Mkuu wa UN aunga mkono mapatano ya JCPOA
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatima isiyofahamika ya mapatano ya JCPOA kutokana na ukwamishaji wa Marekani na kuunga mkono mapatano hayo.
Rosemary DiCarlo ametangaza baada ya kumalizika kikao cha Baraza la Usalama la UN kwamba mapatano ya JCPOA ndiyo njia bora zaidi ya kudhamini amani na kuendeleza kwa njia ya amani miradi ya nyuklia ya Iran licha ya changamoto zilizopo.
Bi DiCarlo ameongeza kuwa, ni jambo la dharura kufungamana kikamilifu na mapatano ya JCPOA na kutekeleza kikamilifu azimio nambari 2231 kwa ajili ya amani na usalama wa eneo la magharibi mwa Asia. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaja hatua ya Marekani ya kujitoa kwenye mapatano hayo mwaka 2018 kuwa ni pigo kwa mapatano hayo na kueleza kuwa inasikitisha mapatano hayo kuwa na hatima isiyofahamika.
Kikao cha Baraza la Usalama la UN kilifanyika jana usiku kwa njia ya video kwa ajili ya kuchunguza ripoti ya tisa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu matukio ya karibuni ya utekelezaji wa azimio nambari 2231. Nchi wanachama wa Baraza la Usalama, isipokuwa Marekani, zimeunga mkono kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kukosoa hatua za upande mmoja za Marekani za kuiwekea Iran vikwazo na kujitoa kwenye mapatano hayo.
Nchi hizo zimesisitiza kuwa kurefushwa muhula wa marufuku ya silaha dhidi ya Iran kwa mujibu wa kile kilichowasilishwa na Marekani ni kinyume na mapatano ya JCPOA na ni ukiukaji wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Marufuku ya silaha dhidi ya Iran itaondolewa tarehe 18 mwezi Oktoba mwaka huu kwa mujibu wa kipengee cha azimio 2231 la Baraza la Usalama.