Abdullah Abdullah: Mazungumzo ya amani na Taliban ni magumu
(last modified Sat, 19 Sep 2020 04:28:29 GMT )
Sep 19, 2020 04:28 UTC
  • Abdullah Abdullah: Mazungumzo ya amani na Taliban ni magumu

Mkuu wa Baraza la Maslahi ya Taifa la Afghanistan amesema, mazungumzo ya amani baina ya Waafghani wanayofanya wao na kundi la Taliban ni magumu.

Abdullah Abdullah amesisitiza kuwa, mazungumzo hayo yanayofanyika Doha, mji mkuu wa Qatar hayatokuwa ya mepesi na kwamba serikali ya Afghanistan itakabiliwa na masuala kadhaa ambayo ni vigumu kuyatolea maamuzi.

Hata hivyo mkuu huyo wa Baraza la Maslahi ya Taifa la Afghanistan ametoa hakikisho kwamba, kupitia mazungumzo hayo haki za raia, haki za wanawake na haki za binadamu zitalindwa; na uhuru na uadilifu utadhaminiwa kwa ajili ya watu hao.

Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai ambaye amekutana na kufanya mazungumzo na Abdullah Abdullah amesema, anaunga mkono kuanza mazungumzo ya amani baina ya Waafghanistan na akaeleza kwamba, pande mbili za serikali na Taliban zinapaswa kuitumia fursa iliyojitokeza kuhitimisha vita nchini humo.

Abdullah Abdullah (anayeangalia kamera) akiongoza ujumbe wa serikali katika mazungumzo ya amani ya Doha

Wakati huohuo Moulavi Abdulhakim, kiongozi wa ujumbe wa Taliban katika mazungumzo ya amani ya Doha amethibitisha kuwa, pande husika katika mazungumzo, jana Ijumaa zilikutana kwa siku ya pili mfululizo kwa majadiliano ya ana kwa ana.

Mazungumzo ya kutafuta suluhu na kurejesha amani nchini Afghanistan yalianza rasmi siku ya Jumamosi ya tarehe 12 Septemba huko mjini Doha, Qatar kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa serikali na wa kundi la Taliban pamoja na wajumbe wa nchi kadhaa duniani.

Miongoni mwa ajenda kuu za mazungumzo hayo ni aina ya mfumo ujao wa kisiasa wa Afghanistan, usitishaji vita, haki za jamii za waliowachache, uhuru wa kutoa maoni na wa vyombo vya habari, haki za wanawake na mafanikio yaliyopatikana nchini humo katika miongo miwili ya karibuni.../

Tags