Kasi kubwa ya maambukizi ya COVID-19 yazusha taharuki barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64545-kasi_kubwa_ya_maambukizi_ya_covid_19_yazusha_taharuki_barani_ulaya
Ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona na ugonjwa wa COVID-19 barani Ulaya na uhaba wa vifaa vya kukabiliana na maambukizi vilimezidisha taharuki katika nchi za bara hilo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Nov 10, 2020 08:27 UTC
  • Kasi kubwa ya maambukizi ya COVID-19 yazusha taharuki barani Ulaya

Ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona na ugonjwa wa COVID-19 barani Ulaya na uhaba wa vifaa vya kukabiliana na maambukizi vilimezidisha taharuki katika nchi za bara hilo.

Taasisi ya Robert Koch ya Ujerumani imeripoti kwamba, zaidi ya Wajerumani 13,363 wameambukizwa virusi vya corona katika masaa 24 yaliyopita na 63 kati yao wameaga dunia kutokana na virusi hivyo. 

Ripoti zinasema kuwa, kutokana na kasi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani vitengo vya wagonjwa mahututi katika hospitali za nchi hiyo vimejaa wagonjwa, na kwamba hata vitengo vya huduma za dharura havina tena uwezo wa kupokea wagonjwa wapya.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) pia zinaonyesha kuwa, idadi ya wagonjwa wa COVID-19 nchini Uingereza imevuka watu milioni moja na laki mbili na 13 elfu na wahanga wa ugonjwa huo wamefikia karibu elfu 50. 

Katika jamhuri ndogo ya Latvia yenye jamii ya watu milioni mbili, kumetangazwa hali ya hatari kutokana na kasi ya maambukizi ya corona. Hii ni mara ya pili kutangazwa hali ya hatari kaika nchi hiyo kutokana na virusi vya corona. 

Huko katika Jamhuri ya Czech serikali imeanza kutumia wanajeshi kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya kukabiliana na maambukizi ya corona. WHO inasema kuwa idadi ya wagonjwa wa corona katika nchi hiyo imepindukia watu laki nne na 20 elfu na karibu elfu tano miongoni mwao wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo. 

Huko Ufaransa ambayo inashika nafasi ya kwanza barani Ulaya na ya tano duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya corona, zaidi ya watu milioni mbili laki 8 na 79 elfu na 479 wameambukizwa virisi vya corona na karibu elfu 41 miongoni mwao wameaga dunia. 

Italia imezidisha sheria za kukabiliana na corona zitakazoanza kutekelezwa kesho Jumatano huku vyombo husika vikizidisha juhudi za kudhibiti maambukizi.

Marekani bado inaongoza duniani kwa kuwa na zaidi ya wagonjwa milioni kumi wa virusi vya corona. Wamarekani zaidi ya laki mbili na 44 elfu pia wameaga dunia kutokana na ugojwa wa COVID-19.

Idadi ya wagonjwa wa corona kote duniani imepindukia watu milioni 51 la laki tatu na nusu, na vifo vya wahanga wa ugonjwa huo vimepindukia milioni moja laki mbili na 71 elfu na 332.

Habari inayotia matumaini katika uwanja huu ni ile ya afanikio ya chanjo ya makampuni ya Pfizer na BioNTech ya chanjo ya virusi vya corona. 

Makampuni hayo yametangaza kuwa chanjo hiyo inakinga virusi ya corona kwa asilimia 90.