UNICEF yataka walimu wapewe kipaumbele katika chanjo ya COVID-19
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65216-unicef_yataka_walimu_wapewe_kipaumbele_katika_chanjo_ya_covid_19
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limetaka walimu wapewe kipaumbele katika chanjo ya COVID-19 au corona.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 16, 2020 03:02 UTC
  • UNICEF yataka walimu wapewe kipaumbele katika chanjo ya COVID-19

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limetaka walimu wapewe kipaumbele katika chanjo ya COVID-19 au corona.

Katika taarifa mkurugenzi mkuu wa UNICEF amesema janga la corona au COVID-19 limevuruga elimu ya watoto kote duniani na kuwachanja waalimu dhidi ya COVID-19 ni hatua muhimu ya kurejesha elimu ya watoto hao katika mkondo unaotakiwa.

Bi. Henrietta Fore amesema katika kilele cha janga hilo mwishoni mwa mwezi Aprili 2020, ufungaji wa shule ulivuruga masomo ya karibu asilimia 90 ya wanafunzi kote duniani. 

Ameongeza kuwa wakati idadi hiyo imeanza kushuka tangu wakati huo lakini “bado kuna dhana kwamba kufunga shule kunaweza kupunguza kusambaa kwa maambukizi licha ya kuongezeka kwa ushahidi kwamba shule sio chachu kubwa ya maambukizi katika jamii.

Kampeni ya kukomesha corona nchini Kenya

Bi. Fore amesisitiza kuwa ingawa maamuzi ya mgawanyo wa chanjo hizo yako mikononi mwa serikali lakini athari za kuendelea kukosa au kutohudhuria masomo ni kubwa sana hususan kwa watu wasiojiweza.

Ametahadharisha kuwa, kadiri watoto wanavyoendelea kuwa nje ya shule , uwezekano wa kurejea unakuwa mgumu.

Amesema anaamini kwamba “Haya ni maamuzi magumu ambayo yanahitaji kuchukua hatua ngumu. Lakini kile ambacho hakipasi kuwa maamuzi magumu ni kufanya kila kilicho ndani ya uwezo wetu, yaani kulinda mustakabali wa kizazi kijacho na hii inaanza kwa kuwalinda wale wanaohusika kwa kufungua mlango wa mustakabali huo wa kizazi kijacho.”