Ripoti: Polisi ya Marekani imeua makumi ya Wamarekani weusi tokea 2015
Uchunguzi mpya umefichua kuwa, makumi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika wameuawa na polisi ya nchi hiyo tokea mwaka 2015.
Uchunguzi huo uliofanywa na Radio ya Kitaifa ya Uma (NPR) umefichua kuwa, Wamarekani weusi zaidi ya 135 ambao hawakuwa wamejizatiti kwa silaha yoyote wameuawa na maafisa wa polisi ya nchi hiyo tokea mwaka 2015 hadi sasa.
Ripoti ya uchunguzi huo iliyotolewa jana Jumatatu inaonesha kuwa, asilimia 75 ya maafisa wa polisi waliohusika katika mauaji hayo ni Wamarekani weupe (Wazungu).
Uchunguzi huo umebainisha kuwa, zaidi ya kesi 80 za mauaji hayo hazikufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, huku kesi 33 za ukatili huo zikipelekea maafisa husika wa polisi ama kujiuzulu au kufutwa kazi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya NPR, ni maafisa 13 tu waliohusika na mauaji hayo walifunguliwa mashitaka katika kipindi hicho cha miaka mitano.
Mbali na kusumbuliwa na ukatili wa vyombo vya dola hususan polisi na askari usalama, Wamarekani weusi wanaandamwa pia na ubaguzi wa rangi, ubaguzi katika sekta ya elimu, ajira na katika masuala ya kijamii.