UN yazikosoa nchi za Ulaya kwa ukatili dhidi ya wahajiri
Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limezitaka nchi za Ulaya zikomesha ukatikli dhidi ya wahamiaji.
Tovuti ya EUobserver imeripoti kuwa, afisa wa shirika la IOM linalofanya kazi chini ya Umoja wa Mataifa, Eugenio Ambrosi, amesema nchi za Ulaya zinapaswa kukomesha na kuzuia ukatili unaofanywa katika nchi hizo dhidi ya wakimbizi.
Ameongeza kuwa, utumiaji wa mabavu na ukatili dhidi ya raia haukubaliki, na Umoja wa Ulaya unalazimika kuchukua hatua za haraka za kuzuia nchi wanachama kuwafukuza kwa umati wakimbizi na wahajiri.
Ripoti zinasema nchi za Ulaya zimezidisha sera za kuwapiga vita wakimbizi licha ya kupungua wimbi la wahajiri kuelekea katika bara hilo.
Hivi karibuni Gillian Triggs ambaye ni afisa wa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa alieleza wasiwasi wake kuhusu kamatakamata ya wahajiri na wakimbizi wanaoingia katika mipaka ya Ulaya, kuwarejesha nyuma kwa mabavu na bila ya kutilia maanani mahitaji yao ya kibinadamu na kusema kitendo hicho kinakiuka sheria.