Borrell: Nitafanya kila niwezalo kuinusuru JCPOA
(last modified Sun, 21 Mar 2021 03:23:24 GMT )
Mar 21, 2021 03:23 UTC
  • Borrell: Nitafanya kila niwezalo kuinusuru JCPOA

Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema atafanya juu chini ili kuyalinda na kuyabakisha hai makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kwa kifupi kama JCPOA.

Josep Borrell amesema hayo katika kitabu chake kinachoitwa 'Sera za Nje za Ulaya katika Zama za Covid-19.'

Amebainisha kuwa, "kama mshirikishi wa hivi sasa wa JCPOA, nitaendelea kushirikiana na wadau wengine wa makubaliano hayo pamoja na jamii yote ya kimataifa. Tutafanya kila liwezekanalo kulinda mafanikio tuliyoyapata miaka mitano iliyopita, na kuhakikisha kuwa mapatano hayo yanasalia athirifu."

MKuu huyo wa sera za nje wa EU ameeleza bayana kuwa, makubaliano ya JCPOA yapo chini ya mashinikizo makubwa kutoka pande mbalimbali hususan baada ya Marekani kujiondoa kwayo Mei mwaka 2018, na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran chini ya stratejia mpya ya 'mashinikizo ya kiwango cha juu.'

Mwezi uliopita, mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa EU alikiri kuwa, hadi kufikia wakati ambao Marekani ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika JCPOA, Iran ilikuwa inafungamana na mapatano hayo na kwamba hata baada ya hapo iliendelea kufungamana na mapatano hayo.

Baada ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuiondoa Washingtonkatika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 2018, nchi za Ulaya hazikuchukua hatua yoyote ya maana ya kuyalinda mapatano hayo. Nchi hizo za Ulaya zilikuwa zikidai mara kadhaa kuwa kwa kuzingatia kwamba mapatano ya JCPOA ni muhimu katika kulinda usalama wa kieneo na kimataifa zilitaka mapatano hayo yaendelee kuwepo na kuahidi kuyalinda.

Tags