Muslim Advocates yaitaka Facebook ikomeshe chuki dhidi ya Uislamu
Taasisi ya Muslim Advocates imewasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya Facebook, Mkurugenzi Mtendaji wake, Mark Zuckerberg na kiongozi nambari mbili wa kampuni hiyo, Sheryl Sandberg ikiitaka Facebook kutilia maanani harakati zinazoeneza chuki na uhasama dhidii ya Waislamu katika mtandao huo.
Ujumbe wa Muslim Advocates umesema: "Tumewasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya Facebook baada ya kampuni hiyo kutotimiza ahadi yake ya kuondoa matangazo yote yanayochochea chuki na uhasama dhidi ya Waislamu."
Muslim Advocates imesema kuwa katika kipindi cha miaka 8 iliyopita Facebook ilijulishwa kuhusu makumi ya mifano ya uchochezi wa chuki na uhasama dhidi ya Waislamu katika kurasa zake lakini haikuchukua hatua yoyote.
Mwaka 2013 maafisa wa Muslim Advocates walikutana na wakuu wa Facebook akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mark Zuckerberg ili kuwaelimisha juu ya hatari ya matangazo na makala zinazochochea chuki dhidi ya Uislamu katika mtandao huo lakini kampuni hiyo haikuchukua hatua.

Vilevile mwishoni mwa mwaka 2019 Muslim Advocates iliikabidhi Faceboon orodha yenye majina ya makundi 26 yanayoeneza chuki dhidi ya Uislamu katika mtandao huo na kwamba 19 kati ya makundi hayo yangali yanaendesha harakati hizo katika Facebook. Orodha hiyo inajumuisha makundi kama "Harakati ya Kupinga Uislamu", "Utakaso wa Ulimwengu", "Uislamu ni Uovu Mtupu."