Maelfu waandamana katika bandari ya Oakland, Marekani kuiunga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i70914-maelfu_waandamana_katika_bandari_ya_oakland_marekani_kuiunga_mkono_palestina
Maandamano ya maelfu ya watu ya kuiunga mkono Palestina na kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina yamefanywa kwa kushirikiana na Muungano wa Wafanyakazi wa Bandari za Marekani. Maandamano hayo yamefanikiwa kuzuia meli ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukaribia bandari hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2021 02:28 UTC
  • Maelfu waandamana katika bandari ya Oakland, Marekani kuiunga mkono Palestina

Maandamano ya maelfu ya watu ya kuiunga mkono Palestina na kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina yamefanywa kwa kushirikiana na Muungano wa Wafanyakazi wa Bandari za Marekani. Maandamano hayo yamefanikiwa kuzuia meli ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukaribia bandari hiyo.

Maandamano hayo ambayo yamefanyika kwa ajili ya kutetea na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina yameizuia meli ya Kampuni ya ZIM ya Israel kupakua mizigo katika Bandari ya Oakland. 

Wakati huo huo televisheni ya NBC ya Marekani imeripoti kuwa, karibu waandamanaji elfu moja wameilazimisha meli ya kampuni ya ZIM ya Israel kwenda mbali na bandari hiyo.  

Maandamano hayo yamefanyika baada ya Muungano wa Wafanyakazi wa Bandari nchini Marekani kutangaza mshikamano wao mkubwa na watu wa Palestina.    

Msemaji wa maandamano hayo Wassim Hage amesema kuwa  wameitisha maandamano kama sehemu ya jitihada za kuwaunga mkono Wapalestina katika kutetea ardhi zao zilizoghusubiwa na Israel na kupinga mauaji ya kizazi yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wasio na hatia.  

Maandamano ya kuiunga mkono Palestina katika bandari ya Oakland 

Hage ameongeza kuwa, wamechukua hatua hiyo pia kama sehemu ya mwito wa kimataifa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kuzizuia meli za kampuni ya ZIM yenye mfungamano na Israel kupakua mizigo yake popote pale.

Maandamano na hatua sawa na hizo zilizochukuliwa katika Bandari ya Oakland zinatazamiwa pia kushuhudiwa huko Los Angeles, Vancouver, Houston, Seattle/Tacoma, New York, Italia na Afrika Kusini.