Peskov: Hakuna uwezekano wa kutokea vita vya tatu vya dunia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i71910-peskov_hakuna_uwezekano_wa_kutokea_vita_vya_tatu_vya_dunia
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia "Kremlin" amesema, katika mazingira ya sasa ya kuendelea kulindwa mlingano wa silaha za nyuklia hakuna uwezekano wa kuanza vita vikuu vya tatu vya dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2021 05:04 UTC
  • Dmitry Peskov
    Dmitry Peskov

Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia "Kremlin" amesema, katika mazingira ya sasa ya kuendelea kulindwa mlingano wa silaha za nyuklia hakuna uwezekano wa kuanza vita vikuu vya tatu vya dunia.

 

Dmitry Peskov ambaye alikuwa akijibu swali kuhusu uwezekano wa kuanza vita kuu ya tatu ya dunia kwa kutumia silaha za nyuklia, amesema kwamba, Rais Vladimir Putin wa Russia ameeleza bayana kwamba, ni jambo lililo mbali sana kutokea vita hivyo. 

Msemaji wa Kremlin ameongeza kuwa, suala la kulindwa mlingano wa nguvu za nyuklia lina umuhimu mkubwa sana katika uwanja huu, kwa sababu linasaidia kuimarisha utulivu wa kistratijia wa sasa duniani. Amesema japokuwa kuna baadhi ya nchi zinazofanya jitihada za kuvuruga mlingano huo, lakini Russia imechukua hatua za lazima za kujilinda.

Msemaji wa Kremlin amesema miongoni mwa hatua hizo ni kutumia mifumo mipya ya silaha kwa ajili ya kulinda mlingano wa nguvu za nyuklia na kujikinga mkabala wa mshambulizi ya aina yoyote ya Marekani. 

Akizungumza na wananchi wa Russia Jumatano wiki hii, Rais Vladmir Putin alisema hadhani kuwa, tukio la manowari ya jeshi la Uingereza kuingia katika pwani ya Russia katika Bahari Nyeusi linaweza kuwa mwanzo wa vita kuu ya tatu ya dunia, hata kama jeshi la Russia lingelazimika kuzamisha manowari hiyo. 

Vladmir Putin

Putin alisema kuwa, kitendo cha manowari ya jeshi la Uingereza ya HMS Defender cha kuingia kinyume cha sheria katika maji ya Russia kilikuwa cha kichochezi.