WSJ: Marekani kuondoa askari wake Iraq kufikia mwishoni mwa 2021
Gazeti la Kimarekani la Wall Street Journal limedai kuwa, Marekani na Iraq zimeafikiana juu ya kuondoka wanajeshi wote wa US kutoka katika nchi hiyo ya Kiarabu kufikia mwishoni mwaka huu 2021.
Gazeti hilo limenukuu duru za kuaminika zinazodai kuwa, viongozi wa Washington na Baghdad karibu hivi watatoa taarifa ya pamoja juu ya kuondoka askari hao vamizi nchini Iraq kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Ripoti ya WSJ imedai kuwa, taarifa hiyo ya pamoja ya Washington na Baghdad hata hivyo itasisitiza kuwa Iraq ingali inahitaji ushirikiano wa kiitelijensia na mafunzo ya kijeshi na jeshi la Marekani.
Hii ni katika hali ambayo, Fouad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ameliambia gazeti la Wall Street Journal kuwa, Iraq haiwahitajii askari wa Marekani kwa kuwa nchi hiyo ya Kiarabu ina wanajeshi wake.
Akthari ya wananchi wa Iraq wanataka vikosi vya wanajeshi vamizi wa Marekani viondoke katika ardhi ya nchi hiyo hususan baada ya Bunge la Taifa la nchi hiyo kutoa agizo likitaka kuondoka wanajeshi wote vamizi nchini Iraq.
Bunge la Iraq lilichukua hatua hiyo siku chache baada ya aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Shahidi Qassem Soleimani, Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu wa Mkuu wa Harakati ya al Hashdu-Sha'abi na wanamapambano wenzao wanane kuuliwa kigaidi na kidhulma na wanajeshi magaidi wa Marekani, katika shambulio la anga lililofanywa na magaidi hao karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq Januari 3, mwaka 2020.