Watoto wa Kiafghani zaidi ya milioni nne hawaendi shule
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeripoti kuwa watoto wa Kiafghani zaidi ya milioni nne hawajajiandikisha kuanza shule mwaka huu nchini humo.
Shirika la Unicef limesema kuwa, asilimia 60 ya watoto ambao hawajajiandikisha kuanza shule ni wa jinsia ya kike na kusisitiza kuwa watoto wa Kiafghani hivi sasa wanasumbuliwa na ukosefu wa maji safi, dawa na chakula cha kutosha. Baada ya kundi la wanamgambo wa Taliban kuwaruhusu wanafunzi wa kiume wa shule za sekondari za elimu ya kati na juu pekee kurejea masomoni; Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetaka taasisi za elimu za nchini Afghanistan ziwaruhusu watoto wa kike pia kuhudhuria masomo na kutahadharisha kuwa hatua hiyo itakuwa na taathira mbaya kwa nusu ya jamii ya nchi hiyo.
Shirika la UNESCO jana liliarifu kuwa, iwapo watoto wa kike wataendelea kuzuiwa kwenda shule huko Afghanistan huo utakuwa ni ukiukaji mkubwa wa haki za msingi za kwenda shule watoto wa kike na wanawake. Shirika la UNESCO limebainisha hayo huku Wizara ya Elimu inayoongozwa na utawala wa kundi la Taliban ikiwa imetoa mwito wa wanafunzi na walimu wa kiume kudhuhuria mashuleni; huku hatima ya kupata fursa ya kusoma watoto wa kike ikiwa haijulikani.