Majirani za Afghanistan wapinga uingiliaji wa kigeni, vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134340-majirani_za_afghanistan_wapinga_uingiliaji_wa_kigeni_vikwazo
Wawakilishi maalum wa nchi majirani za Afghanistan wamepinga vikali uwepo wowote wa kijeshi wa maajinabi, wakizitaka nchi zilizopelekea kushuhudiwa mgogoro wa sasa nchini humo kuchangia ujenzi mpya bila kutumia msaada kama chombo cha kisiasa.
(last modified 2025-12-15T11:34:30+00:00 )
Dec 15, 2025 11:34 UTC
  • Majirani za Afghanistan wapinga uingiliaji wa kigeni, vikwazo

Wawakilishi maalum wa nchi majirani za Afghanistan wamepinga vikali uwepo wowote wa kijeshi wa maajinabi, wakizitaka nchi zilizopelekea kushuhudiwa mgogoro wa sasa nchini humo kuchangia ujenzi mpya bila kutumia msaada kama chombo cha kisiasa.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran mwishoni mwa mkutano wa wawakilishi maalum wa nchi zinazopakana na Afghanistan hapa Tehran imesema kwamba, wawakilishi hao walisisitiza ujumuishaji wa kikanda na umuhimu wa eneo hili katika kutatua masuala na changamoto zilizopo, ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusiana na Afghanistan.

Mkutano huo wa Tehran wa jana Jumapili uliwaleta pamoja maafisa kutoka Iran, Pakistan, Russia, Uzbekistan, China, Tajikistan, na Turkmenistan ili kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Afghanistan na maeneo ya Asia Kusini na Asia ya Kati.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, washiriki walisisitiza umuhimu wa kuimarisha utulivu nchini Afghanistan na kuelezea utayarifu wao wa kusaidia kufanikisha hilo ikiwa Afghanistan itawaomba.

Wamesisitiza haja wa kuboresha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na Afghanistan kwa lengo la kunyanyua maisha ya watu wa nchi hiyo, na kuashiria hitaji la kuunganishwa kwa nchi hiyo katika mifumo ya kisiasa na kiuchumi ya eneo hili.

Kuhusu usalama wa kieneo, wawakilishi hao wametangaza na kusisitiza utayarifu wao wa kusaidia Afghanistan katika kupambana na ugaidi, biashara haramu ya dawa za kulevya, na magendo ya binadamu.

Kadhalika wawakilishi hao wametilia mkazo wajibu wa jamii ya kimataifa wa kuondolewa vikwazo na kuachilia mali zilizozuiliwa za Afghanistan, kuunga mkono kurejeshwa kwa raia wa Afghanistan kutoka nchi jirani, na kuandaa mazingira ya kurejeshwa kwa raia hao kwa heshima.