Umoja wa Mataifa: Tanzania ni rejea ya amani Afrika na duniani kote
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134316-umoja_wa_mataifa_tanzania_ni_rejea_ya_amani_afrika_na_duniani_kote
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Tanzania imekuwa ni rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote.
(last modified 2025-12-15T05:40:22+00:00 )
Dec 15, 2025 02:47 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Tanzania ni rejea ya amani Afrika na duniani kote
    Umoja wa Mataifa: Tanzania ni rejea ya amani Afrika na duniani kote

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Tanzania imekuwa ni rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote.

Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Kombo, pamoja na wenzake kutoka Tanzania.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, taswira ya Tanzania kama kielelezo cha amani ilijaribiwa katika uchaguzi wa hivi karibuni uliofanyika Oktoba 29, 2025, ikiwa ni mara ya kwanza kukabiliwa na changamoto hiyo.

Umoja wa Mataifa ungependa kuona Tanzania inaendelea kubaki katika umoja wake na kuwa mfano bora kwa mataifa mengine,” alisema Katibu Mkuu Guterres alipokuwa akipokea Ujumbe Maalum uliobeba salamu na ujumbe kutoka kwa Rais Samia.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa yenye maana, jumuishi na shirikishi ili kushughulikia chanzo cha matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, pamoja na kutafuta njia za kudumu za kuyazuia yasijirudie tena.

Aidha, aliahidi msaada kamili wa Umoja wa Mataifa wakati wote na hata baada ya Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa nchini Tanzania kukamilisha majukumu yake.

Kwa mujibu wa takwimu za awali zilizotolewa na serikali ni kuwa, katika vurugu za siku tatu zilizotokea kuanzia Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi mkuu jumla ya ofisi za serikali 756 ziliharibiwa, vituo vya mabasi ya mwendo kasi 27, huku mabasi 6 yakiteketezwa kwa moto.

Nyumba binafsi 273, vituo vya polisi 159, na vituo binafsi vya mafuta 672 navyo vilipigwa au kuchomwa moto. Aidha, zaidi ya magari binafsi 1,642 yaliteketezwa, pikipiki 2,268, pamoja na magari ya serikali 976, yakitajwa kuwa miongoni mwa mali zilizoathirika katika machafuko hayo.