Yemen yaonya kuhusu kushtadi jinai za Israel Gaza, Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134334-yemen_yaonya_kuhusu_kushtadi_jinai_za_israel_gaza_ukingo_wa_magharibi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imetahadharisha dhidi ya kuongezeka kwa ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, ikiukosoa utawala huo pandikizi kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kuzidisha mashambulizi.
(last modified 2025-12-15T10:59:22+00:00 )
Dec 15, 2025 10:59 UTC
  • Yemen yaonya kuhusu kushtadi jinai za Israel Gaza, Ukingo wa Magharibi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imetahadharisha dhidi ya kuongezeka kwa ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, ikiukosoa utawala huo pandikizi kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kuzidisha mashambulizi.

Wizara hiyo imesema utawala wa Israel unaendelea na kupanua uchokozi wake dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, huku jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zikibaki kimya na kufumbia macho jinai hizo.

Wakati huo huo, Wizara hiyo imesisitiza msimamo thabiti wa Yemen, katika ngazi ya uongozi wake, serikali na watu wake, katika kuunga mkono taifa la Palestina na haki zao za msingi.

Imeonya kuhusu hatari zinazotokana na kuongezeka kwa uchokozi wa Israel huko Gaza na ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ikitoa mfano wa hivi karibuni wa mauaji ya Raed Saeed Saad, kamanda wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas.

Wizara hiyo imesema uhalifu wa mauaji ya kimbari wa adui Mzayuni dhidi ya Gaza haujakoma na unaendelea kila kukicha, na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya wanawake na watoto.

Wakati huo huo, ofisa mwandamizi wa Hamas, Osama Hamdan, amesema harakati hiyo ina haki ya kujibu ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Wazayuni, hasa mauaji ya kamanda Raed Saad.

Akizungumza na televisheni ya Al Jazeera, kiongozi huyo wa Hamas amesema kwamba, Shahidi Raed Saad "alijitolea kwa ajili ya harakati za Palestina na ulinzi wa ardhi na nchi yake."