Iran: Mvutano Yemen unanufaisha mkakati wa Israel wa kuvuruga Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134298-iran_mvutano_yemen_unanufaisha_mkakati_wa_israel_wa_kuvuruga_asia_magharibi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa tahadhari kali kuhusu mvutano unaoendelea nchini Yemen, ikisema hali hiyo inaunufaisha tu utawala wa Israel na mkakati wake wa kuzigawa nchi za Asia Magharibi au Mashariki ya Kati.
(last modified 2025-12-14T10:00:20+00:00 )
Dec 14, 2025 10:00 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghae
    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghae

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa tahadhari kali kuhusu mvutano unaoendelea nchini Yemen, ikisema hali hiyo inaunufaisha tu utawala wa Israel na mkakati wake wa kuzigawa nchi za Asia Magharibi au Mashariki ya Kati.

Msemaji wa wizara hiyo, Esmaeil Baghaei, alitoa kauli hiyo Jumapili wakati wa mkutano na waandishi wa habari, huku mapigano yakizidi kushika kasi kati ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Saudi Arabia na waasi wanaoshirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu katika kusini mwa Yemen yenye utajiri wa mafuta.

Baghaei alisisitiza kuwa matukio haya yanapaswa kuibua wasiwasi mkubwa kwa mataifa ya eneo, akieleza kuwa mgogoro huo unaenda sambamba na sera za utawala wa Kizayuni za kuzigawa nchi za eneo vipande vipande. Aliongeza kuwa mazungumzo ya dhati kati ya makundi ya Kiyemeni ndiyo njia pekee ya kulinda uthabiti, uhuru na mshikamano wa taifa hilo. Hatua yoyote inayopinda kutoka lengo hilo, alisema, inawanufaisha wale wanaotafuta kuchochea mgawanyiko miongoni mwa mataifa ya Kiislamu na ya kikanda.

Katika mkutano huo, Baghaei pia alijibu swali kuhusu mauaji ya Wamarekani watatu nchini Syria yaliyofanywa na wapiganaji. Alisema tukio hilo halipaswi kushangaza, akieleza kuwa Syria imepoteza sehemu ya ardhi yake kwa muda wa miongo kadhaa, ikiwemo Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel. Aidha, amesema nchi hiyo imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni, hususan katika kipindi cha mwaka uliopita.

Baghaei ameonya kuwa kuendelea kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria, pamoja na uvamizi wa maeneo makubwa ya nchi hiyo na mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani, kunaweza kuzuia juhudi za kurejesha uthabiti na usalama. Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Iran imekuwa ikionya mara kwa mara dhidi ya hatari ya Syria kugeuzwa uwanja wa kuimarisha na kusambaza ugaidi.