Israel yakiri: Tulisababisha uharibifu mdogo kwa Iran kuliko ilivyodhaniwa hapo awali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134238-israel_yakiri_tulisababisha_uharibifu_mdogo_kwa_iran_kuliko_ilivyodhaniwa_hapo_awali
Israel imekiri kuwa ilisababisha uharibifu wa kiwango kidogo kwa Iran wakati wa vita vya siku 12 mwezi Juni mwaka huu kuliko ilivyofikiriwa awali.
(last modified 2025-12-13T02:33:51+00:00 )
Dec 13, 2025 02:33 UTC
  • Israel yakiri: Tulisababisha uharibifu mdogo kwa Iran kuliko ilivyodhaniwa hapo awali

Israel imekiri kuwa ilisababisha uharibifu wa kiwango kidogo kwa Iran wakati wa vita vya siku 12 mwezi Juni mwaka huu kuliko ilivyofikiriwa awali.

Meja jenerali Shlomi Binder Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya jeshi la Israel amemweleza Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Mike Waltz kwamba Israel inaamini kuwa miradi ya makombora ya balistiki ya Iran iliathirika kwa kiasi kidogo katika vita hivyo kuliko ilivyodhaniwa awali. 

Tovuti ya al-Monitor imenukuu chanzo cha karibu na kadhia hii na kueleza kuwa Tel Aviv inaitaka tena Washington kuchukua hatua dhidi ya Iran. 

Chanzo hicho cha karibu kimeongeza  kuwa:" Hili ni tishio ambalo Israel haitaweza kulikubali kwa muda mrefu, na lazima turatibu na Wamarekani mistari nyekundu na hatua tutakazochukua katika siku zijazo, labda hata katika siku za karibuni."

Haya yanajiri huku gazeti la Times of Israel likidai kuwa Iran sasa inamiliki makombora ya balistiki yasiyopungua 2,000; takriban idadi ile ile iliyokuwa nayo usiku wa kuamkia katika vita.” 

Juni 13 mwaka huu Israel ilianzisha vita dhidi ya Iran na kuwauwa shahidi makamanda kadhaa wa ngazi ya juu wa jeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida. 

Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani pia iliingia katika vita hivyo na kushambulia kwa mabomu vituo vitatu vya nyuklia vya Iran huko Fordow, Natanz na Isfahan, katika ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT).

Vikosi vya ulinzi vya Iran pia vilijibu hujuma hiyo ya kichokozi ya Israel na Marekani dhidi ya nchi hii kwa kuyashambulia maeneo ya kimkakati katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na pia kambi ya anga ya Marekani ya al-Udeid huko Doha, Qatar.