Shujaa Muislamu aliyejitolea kupambana na gaidi kuwaokoa Mayahudi Australia + VIDEO
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134330-shujaa_muislamu_aliyejitolea_kupambana_na_gaidi_kuwaokoa_mayahudi_australia_video
Shujaa Muislamu ambaye video yake imeenea mno mitandaoni ikimuonesha akijitolea kwenda katikati ya ufyatuaji risasi na kujikubalisha kupigwa risasi lakini aweze kupambana na kumnyang'anya silaha gaidi aliyekuwa anawafyatulia risasi Mayahudi huko Sydney, anaendelea kupongezwa kote duniani na kuambiwa kwamba ni shujaa ambaye kujitolea kwake kumeweza kuoko maisha ya watu wengi.
(last modified 2025-12-15T06:56:50+00:00 )
Dec 15, 2025 06:56 UTC

Shujaa Muislamu ambaye video yake imeenea mno mitandaoni ikimuonesha akijitolea kwenda katikati ya ufyatuaji risasi na kujikubalisha kupigwa risasi lakini aweze kupambana na kumnyang'anya silaha gaidi aliyekuwa anawafyatulia risasi Mayahudi huko Sydney, anaendelea kupongezwa kote duniani na kuambiwa kwamba ni shujaa ambaye kujitolea kwake kumeweza kuoko maisha ya watu wengi.

Taarifa za karibuni kabisa zinasema kuwa watu wasiopungua 16 wameuawa katika ufyatuaji huo wa risasi huko Sydney, Australia huku video zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zikionesha mwanamme mmoja akipenyapenya katikati ya magari yaliyoegeshwa akimkimbilia mwanamume aliyeshika bunduki, akapambana naye na kumpokonya silaha na baadaye kumuelekezea silaha mshambuliaji huyo ambaye aliamua kukimbia. 

Kisha video hiyo inamuonesha shujaa huyo Muislamu akiwa hana silaha akiendelea kuwafukuza magaidi hao katika jitihada za kuwakingia kifua Mayahudi waliokuwa kwenye sherehe zao za kidini, wasiendelee kupigwa risasi. 

Video inayoonesha harakati za shujaa huyo Muislamu imeenea sana kwenye mitandao ya kijamii, na watumiaji wengi wanamsifu mwanamume huyo kwa ushujaa wake, wakisema matendo yake yameokoa maisha ya watu wengi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Australia, shujaa huyo Muislamu ametambuliwa kwa jina la Ahmed al Ahmed, ana miaka 43 na ni mkazi wa Sydney.

Binamu wa al Ahmed amenukuliwa na televisheni ya Australia akisema kwamba shujaa huyo Muislamu alipigwa risasi mara mbili wakati wa tukio hilo. 

"Yuko hospitalini na hatujui hasa kinachoendelea huko," amesema mtu huyo aliyetambulishwa kwa jina la Mustafa wakati alipohojiwa na televisheni ya Australia na kusema: "Tunatumai atakuwa yuko sawa. Ni shujaa kwa asilimia 100."

Mitandao ya kijamii imejaa pongezi huku mmoja akiandika: "Mtu huyu wa Australia ameokoa maisha ya watu wengi kwa ushujaa wake wa kumpokonya silaha mmoja wa magaidi katika fukwe za Bondi. Huyu ni SHUJAA." 

Chris Minns, Waziri Mkuu wa eneo la New South Wales huko Sydney amesema: "Mtu huyo ni shujaa wa kweli, na sina shaka kwamba kuna watu wengi sana walio hai usiku wa leo kutokana na ushujaa wake."