Maandamano ya fujo yanaendelea nchini Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134324-maandamano_ya_fujo_yanaendelea_nchini_tunisia
Mamia ya watu nchini Tunisia wameendelea kufanya maandamano yaliyoitishwa na vyama vya upinzani na mashirika ya kisheria. Maandamano hayo yanaendelea kwa wiki ya nne mfululizo kwenye mitaa ya mji mkuu Tunis.
(last modified 2025-12-15T06:53:21+00:00 )
Dec 15, 2025 06:53 UTC
  • Maandamano ya fujo yanaendelea nchini Tunisia

Mamia ya watu nchini Tunisia wameendelea kufanya maandamano yaliyoitishwa na vyama vya upinzani na mashirika ya kisheria. Maandamano hayo yanaendelea kwa wiki ya nne mfululizo kwenye mitaa ya mji mkuu Tunis.

Taarifa ya shirika la habari la AFP imesema kuwa, waandamanaji walipaza sauti zao wakisema: "Tunataka wafungwa waachiliwe huru" na "Hatutaki kuwa na jimbo la polisi hapa" ikiwa ni kupinga hatua ya Rais Kais Saied ya kuimarisha hatua za kiusalama nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waandamanaji wamelaani hukumu nzito iliyotolewa ya kesi iliyopewa jina la njama dhidi ya usalama wa taifa na kifungo cha miaka 12 jela dhidi ya Abir Moussa, kiongozi wa Chama cha Katiba Huru nchini Tunisia.

Mawakili wa Tunisia wameitaja hukumu hiyo kuwa ni ya kisiasa na wanaiona ni sehemu ya unyanyasaji wa mfumo wa mahakama ili kuwafuta wapinzani wa kisiasa wa Rais Kais Saied.

Wamesisitiza kwamba Abir Moussa anakabiliwa na kesi nyingine zilizobuniwa dhidi yake ambazo zimetumia chaka la sheria zenye utata kama sheria inayoitwa "Kanuni ya 54" kuhusu kupambana na "taarifa bandia."

Amri ya "Sheria ya 54", ambayo wapinzani wanasema inatumika vibaya kuzuia uhuru wa kujieleza, pia imelalamikiwa vikali na waandamanaji hao.

Washiriki wa maandamano hayo walibeba picha za wanasiasa na wanaharakati kadhaa waliofungwa jela nchini humo na kusisitiza kwamba kupunguzwa uhuru wa kujieleza kumeleta udikiteta wa kisiasa nchini Tunisia. 

Taarifa zinasema kuwa, watu 21 wamekamatwa kwenye jimbo la Kairouan nchini Tunisia baada ya maandamano yaliyofanyika usiku kucha. Maandamano hayo yamechochewa na kifo cha kijana mmoja anayeitwa "Naim Al-Breiki." 

Familia yake inasema kwamba, kijana wao huyo alikuwa anafukuzwa na polisi wakati alipokuwa akiendesha pikipiki na baada ya kugongwa na gari la maafisa usalama na kupigwa, alivuja damu ndani na kuvunjika fuvu la kichwa na kufariki dunia hospitalini.