Bei ya chakula duniani imepanda kwa kiwango cha kutisha
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limesema bei ya chakula duniani imepanda kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
FAO ilisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, bei ya bidhaa muhimu za chakula duniani kwa mwezi wa pili mfufulizo kufikia mwezi uliopita wa Septemba, ilipanda kwa kiwango cha kutia wasi wasi.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika hilo la Umoja wa Mataifa, mwezi uliopita wa Septemba, bei ya chakula duniani ilinakili wastani wa alama 130.0, kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa tokea mwaka 2011.
Takwimu hizo za FAO zimeashiria pia kuwa, bei ya chakula duniani imeongezeka kwa asilimia 32.8, ikiwekwa katika mizani ya mwaka mmoja hadi mwaka mwigine.
Kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, bei ya nafaka duniani ilipanda kwa asilimia 2.0 mwezi uliopita, ikilinganishwa na mwezi wa kabla yake, huku bei ya mafuta ya kupikia ikipanda kwa asilimia 1.7.
Shirika la FAO limesema ongezeko la bei za vyakula duniani limewaathiri zaidi wale ambao kipato chao pia kimepungua kutokana na janga la virusi vya Corona.
Wakati huo huo, FAO imesema kiwango cha uzalishaji wa nafaka mwaka huu kitaongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia tani bilioni 2.800, katika hali ambayo makadirio ya mwezi uliopita ya shirika hilo la UN yalikuwa tani bilioni 2.788.