FAO: Nchi 33 za Afrika zinahitaji msaada wa chakula kutoka nje
(last modified Sat, 16 Mar 2024 07:20:47 GMT )
Mar 16, 2024 07:20 UTC
  • FAO: Nchi 33 za Afrika zinahitaji msaada wa chakula kutoka nje

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema katika ripoti yake mpya kwamba, nchi 45 duniani, zikiwemo 33 za Afrika zinahitaji msaada wa dharura wa chakula kutoka nje.

FAO imesema hayo katika ripoti yake mpya na kueleza kuwa, nchi 33 za Afrika, 9 za Asia, 2 za Amerika ya Latini na eneo la Caribbean na moja ya Ulaya zina uhitaji mkubwa wa msaada wa chakula kutoka nje ya nchi hizo.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema hali hiyo ya nchi 45 duniani kukumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula imesababishwa na migogoro ya kieneo, hali mbaya ya hewa na taathira za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO, takriban watu milioni 700, yaani asilimia 10 ya idadi ya watu duniani, wanalala njaa kila usiku.

UN imesema mifumo ya chakula duniani kuanzia shambani hadi mezani imesambaratika na kusababisha zaidi ya watu bilioni tatu wakose mlo wenye lishe na zaidi ya milioni 700 hawana chakula.

Aidha ripoti ya hivi karibuni kabisa ya Umoja wa Mataifa kuhusu 'Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani' (SOFI) iligundua kuwa idadi kubwa ya watu wasio na lishe bora duniani wanaishi barani Asia ambako takriban watu milioni 425 walikumbwa na njaa mwaka 2021. Hata hivyo tunapoangalia kiwango cha njaa tutaona kuwa ni kikubwa zaidi barani Afrika, huku watu milioni 278 wakiathiriwa na njaa barani humo mwaka 2022.

Mkutano wa tatu wa mabunge kwa ajili ya kukabiliana na njaa duniani umepangwa kufanyika barani Afrika mwaka 2026 ili kutathmini maafikiano yaliyofikiwa huko Chile. 

Tags