Zaidi ya askari 1,300 wa DRC wahamishwa kutoka Goma
(last modified Sat, 17 May 2025 07:26:56 GMT )
May 17, 2025 07:26 UTC
  • Zaidi ya askari 1,300 wa DRC wahamishwa kutoka Goma

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetangaza kuwa, limewahamisha zaidi ya wanajeshi na polisi 1,300 wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutoka kwenye mji wa mashariki wa Goma unaodhibitiwa na waasi wa M23.

Taarifa ya shirika hilo imeeleza kuwa, hadi kufikia siku ya Alhamisi, watumishi 1,359 wa vyombo vya dola waliokuwa wameomba hifadhi kwenye kambi za ujumbe wa kimataifa wa kulinda amani nchini Congo, MONUSCO, walikuwa wameshahamishwa pamoja na familia zao na kupelekwa mji mkuu Kinshasa.

Ripoti ya shiriika hilo inasema kuwa, operesheni hiyo ilikuwa "ngumu" na ilihusisha mashauriano marefu kati yake, serikali, ujumbe wa MONUSCO pamoja na kundi la waasi wa M23.

Kundi la M23, lililo katikati ya mzozo wa mashariki mwa Kongo, limeongeza mashambulizi yake tangu Desemba, likiteka miji muhimu ikiwemo Goma na Bukavu.

Kinshasa na wengine wanailaumu Rwanda jirani kwa kuwaunga mkono M23 — madai ambayo Kigali inakanusha.

Mwezi Machi, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame walikubaliana usitishaji mapigano katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Emir wa Qatar huko Doha. Licha ya makubaliano hayo, mapigano yameendelea katika maeneo ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Mwezi Aprili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner na mwenzake wa Rwanda Olivier Nduhungirehe walisaini tamko lililosimamiwa na Marekani huko Washington, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akihudhuria tukio hilo.