Kuporomoka ushawishi wa Ufaransa Afrika Kaskazini
Kufuatia kuongezeka mvutano wa kidiplomasia kati ya Ufaransa na Algeria, Paris imechukua uamuzi wa kuwafukuza wanadiplomasia wa Algeria walio na hati za kusafiria za kidiplomasia zisizo na visa kujibu mapigo kwa uamuzi wa Algeria wa kuwafukuza wanadiplomasia 15 wa Ufaransa.
Baada ya kumuita balozi mdogo wa Algeria, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilisema katika taarifa yake: "Ufaransa ina haki ya kuchukua hatua zaidi kulingana na jinsi hali inavyoendelea."
Mvutano wa hivi karibuni wa kidiplomasia kati ya Ufaransa na Algeria, ambao uliishia kwa kufukuzwa wanadiplomasia, sio mgogoro wa muda na wa mpito bali ni dhihirisho la mgogoro wa kimuundo katika uhusiano wa baada ya ukoloni wa Ufaransa na makoloni yake ya zamani.
Mgogoro huu unaonyesha kwamba, Paris sio tu kwamba, imeshindwa kufafanua upya nafasi yake katika Afrika Kaskazini, lakini pia inapoteza kwa kasi ushawishi wake wa kijiografia Afrika nzima.
Mzozo huu mpya uliibuka hivi majuzi baada ya uamuzi wa serikali ya Algeria wa kuwafukuza wanadiplomasia 15 wa Ufaransa kutokana na kuwepo kwao "haramu" katika ardhi ya nchi hiyo. Uamuzi ambao mara moja umekabiliwa na radiamali ya Wafaransa, ambao wamejibu mapigo kwa kuwafukuza wanadiplomasia wa Algeria ambao walikuwa na pasipoti za kidiplomasia bila visa.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, katika mahojiano nadra na mtandao wa BFM, alisema kwa uwazi kwamba uhusiano wa pande mbili na Algeria "umefungwa kabisa"; maneno ambayo yanachukuliwa kuwa ishara ya kusambaratika njia zote rasmi za kidiplomasia baina ya nchi mbili hizo.
Katika mgogoro huu, kuna mambo mawili muhimu yanajitokeza: Mosi, ni ukali wa hatua za kukabiliana na pili ni uzembe katika kutangaza kikwazo halisi cha mahusiano.
Mambo haya mawili yanaonyesha wazi kuwa mgogoro huo ni zaidi ya mvutano wa kidiplomasia na yanaonyesha mpasuko mkubwa zaidi katika uhusiano wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili.
Ufaransa na Algeria zina historia ya pamoja katika miaka 200 iliyopita, inayofungamana na ukoloni, vita, na utegenmezi wa kila mmoja kwa mwenzake.
Katika miezi ya hivi karibuni, mambo yameharibika zaidi baada ya uhusiano kati ya Algeria na Ufaransa kuingia tena katika mgogoro kiasi kwamba, uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili pia umeathiriwa na hali hiyo ambapo idadi ya wanadiplomasia kutoka nchi hizo mbili wamefukuzwa, jambo ambalo lina mizizi katika historia ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Waalgeria katu hawawezi kusamehe au kusahau uhalifu wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika, hasa kwa kuwa maafisa wa Ufaransa kamwe hawajaomba msamaha wala kulipa fidia kwa Waalgeria. Ingawa Ufaransa imefanya uhalifu mkubwa zaidi na mauaji ya kimbari nchini Algeria, na nyaraka za kihistoria za uhalifu huu zinathibitisha hilo, lakini maafisa wa Paris daima wamekuwa wakikwepa kuomba radhi na badala yake wamekuwa wakitaka kuweko utendaji wenye mtazamo wa mustakabali.
Mzozo wa Algeria na Ufaransa unaongezeka wakati ambapo Ufaransa sio tu inapuuzilia mbali historia yake ya kikoloni huko Algeria bali pia katika miezi ya hivi karibuni imechukua hatua ambazo zimeongeza hasira ya Waalgeria.
Moja ya mambo muhimu yanayochangia pakubwa kushadidi mvutano wa hivi karibuni ni msimamo wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu Sahara Magharibi. Algeria kwa muda mrefu imekuwa mfuasi wa Harakati ya Polisario na ilipinga kunyakuliwa Sahara Magharibi na Morocco, lakini mwaka 2022, Ufaransa iliunga mkono mpango wa Morocco, hatua ambayo iliikasirisha Algeria.
Suala hili si tu kwamba ni mzozo wa kididoplomasia, bali pia ni changamoto ya kimkakati kwa Algeria, kwani linaimarisha ushawishi wa Ufaransa nchini Morocco na kuvuruga uwiano wa nguvu katika eneo hilo.
Sera za uhamiaji za serikali ya Ufaransa pia zimechangia pakubwa katika kuzidisha mzozo huo. Kupunguzwa hisa ya viza kwa raia wa Algeria na shinikizo la kuwatimua wahajiri haramu hususan katika muktadha wa sera za udhibiti wa uhamiaji za Macron kumekabiliwa na jibu hasi kutoka kwa Algeria.

Hatua hizi hazikuonekani tu kama kichocheo cha shinikizo la kisiasa, lakini zinakumbusha uhusiano wa kibabe na kupenda kujitanua wa enzi ya ukoloni, ambapo Ufaransa iliamiliana vibaya mno na raia wa Afrika Kaskazini.
Katika hali ambayo, Paris inajaribu kuimarisha nafasi yake katika mwambao wa kusini mwa bahari ya Mediterania, mgogoro huu unaweza kusababisha kudhoofika nafasi ya Ufaransa katika milingano ya Afrika Kaskazini na Umoja wa Afrika.
Katika miaka ya hivi karibuni, Ufaransa imekabiliwa na kupromoka ushawishi wake katika eneo la Afrika Magharibi. Mapinduzi ya Mali, Burkina Faso na Niger na kutimuliwa wanajeshi wa Ufaransa kutoka Afrika Magharibi, kulionyesha kuwa nchi nyingi za Kiafrika haziko tayari tena kukubali sera za Paris.
Ikiwa Algeria nayo itaelekea kikamilifu upande wa China na Russia, au hata Uturuki, hiyo itakuwa na maana ya pigo jingine na kushindwa kwingine kimkakati Ufaransa, mara hii ikiwa ni huko Afrika Kaskazini.