Kiongozi Muadhamu: Matamshi ya Trump ni fedheha kwa taifa la Marekani
(last modified Sat, 17 May 2025 11:23:33 GMT )
May 17, 2025 11:23 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Matamshi ya Trump ni fedheha kwa taifa la Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amekosoa matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani na kuyataja kuwa ni "fedheha" kwa taifa la Marekani.

"Matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani wakati wa ziara yake katika eneo hili ni fedheha kwa mzungumzaji (Trump) na fedheha kwa taifa la Marekani," Ayatullah Khamenei amesema hayo leo hapa Tehran alipokutana na kundi la walimu na wakufunzi kutoka kote nchini.

Kiongozi Muadhamu amesema Marekani imetumia uwezo wake si kwa ajili ya amani bali kuua watoto na watu wa Gaza, kinyume na alivyodai Trump. "Trump alisema alitaka kutumia mamlaka kwa ajili ya amani; alidanganya," Ayatullah Khamenei amesisitiza.

"Yeye (Trump) na maafisa wa Marekani, utawala wa Marekani, wametumia uwezo wao kuua Gaza, kuchochea vita popote walipoweza, na kuwaunga mkono mamluki wao."

Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa, hata hivyo madaraka yanaweza kutumika kwa ajili ya amani na usalama na ndiyo maana Jamhuri ya Kiislamu inajitahidi kila siku kuimarisha uwezo na nguvu zake. "Lakini hawakufanya hivyo," amesema Kiongozi Muadhamu na kuongeza kuwa, "Walitumia uwezo wao kuupa utawala wa Kizayuni mabomu ya tani kumi ili kuwadondoshea watoto wa Gaza, hospitali, makazi ya watu, huko Lebanon na popote walipoweza."

Kwa mujibu wa Ayatullah Khamenei, Rais wa Marekani anazipa nchi za eneo za Kiarabu mfano ambao, kwa maneno yake mwenyewe, nchi hizi haziwezi kuishi bila Marekani kwa hata siku kumi.

"Mtindo huu kwa hakika umeshindwa," Kiongozi Muadhamu amebainisha. "Kutokana na mapambano ya mataifa ya kikanda, Marekani lazima na itaondoka katika eneo hili," Imam Khamenei ameeleza bayana.

Ayatullah Khamenei pia ameutaja utawala wa Israel kuwa ni "chimbuko la ufisadi, chanzo cha vita na mzizi wa hitilafu" katika eneo la Asia Magharibi na kuongeza kuwa, "Utawala wa Kizayuni, ambao ni uvimbe hatari na mbaya wa saratani katika eneo hili, lazima ung'olewa na hakuna shaka utang'olewa."