Kiongozi wa Mapinduzi aipongeza timu ya miereka kwa kutwaa ubingwa wa dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130916-kiongozi_wa_mapinduzi_aipongeza_timu_ya_miereka_kwa_kutwaa_ubingwa_wa_dunia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameipongeza timu ya taifa ya Iran ya mchezo wa miereka ya freestyle kwa kutwaa taji la ubingwa wa dunia katika Mashindano ya Miereka ya Dunia ya 2025 yaliyofanyika mjini Zagreb, Croatia.
(last modified 2025-09-17T13:51:28+00:00 )
Sep 17, 2025 13:51 UTC
  • Kiongozi wa Mapinduzi aipongeza timu ya miereka kwa kutwaa ubingwa wa dunia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameipongeza timu ya taifa ya Iran ya mchezo wa miereka ya freestyle kwa kutwaa taji la ubingwa wa dunia katika Mashindano ya Miereka ya Dunia ya 2025 yaliyofanyika mjini Zagreb, Croatia.

Katika ujumbe wake huo, Ayatullah Khamenei amepongeza kujitolea kunakostaajabisha na mwenendo wa kustahiki pongezi kubwa ulioonyeshwa na mabingwa hao wa miereka ya freestyle.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "natoa shukrani zangu kwa timu ya miereka bingwa wa dunia kwa juhudi zao za kustaajabisha na mwenendo wao wa kupendezesha. Mchanganyiko wa nguvu na umaanawi hujenga tunu adhimu. Nakupeni heko!".

Siku ya Jumatatu, Timu ya Taifa ya Miereka ya Freestyle ya Iran ilitwaa taji la ubingwa katika Mashindano ya Dunia ya Miereka ya 2025 huko Zagreb, Croatia, na kujinyakulia ushindi wake wa kwanza baada ya kupita kipindi cha miaka 12.

Timu hiyo ilimaliza mashindano hayo ikiwa na medali mbili za dhahabu, mbili za fedha na tatu za shaba, na jumla ya alama 145, ikiiacha nyuma timu ya miereka ya Marekani.

Wanamiereka wa Iran waliofanya vizuri sana katika mashindano hayo ni pamoja na  Amirhossein Zareh, ambaye ametwaa medali ya dhahabu katika uzito wa kilo 125, na Ahmad Mohammadnejad-Javan, ambaye amenyakua medali ya fedha katika uzito wa kilo 61.

Medali za shaba zimekwenda kwa Mohammad Nokhodi (kilo 79), Kamran Ghasempour (kilo 86), na Amirhossein Firoozpour (kilo 92).

Mnamo siku ya Jumanne iliyotamatisha mashindano hayo, Rahman Amouzad alishinda medali ya dhahabu katika kilo 65, naye Amirali Azarpira alinyakua medali ya fedha katika kilo 97.

Ushindi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashindano ya dunia ya Zagreb, umefufua tena kumbukumbu za ushindi wake katika mashindano ya dunia ya mchezo wa miereka iliowahi kutwaa mara tano kuanzia mwaka 1961, 1965, 1998, 2002 na 2013.../