Watoto nusu milioni waingia hatarini kutoka na ghasia mjini Tripoli Libya
(last modified Fri, 16 May 2025 02:22:21 GMT )
May 16, 2025 02:22 UTC
  • Watoto nusu milioni waingia hatarini kutoka na ghasia mjini Tripoli Libya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kuwa, kuongezeka ghasia ndani na karibu na mji mkuu wa Libya, Tripoli, kunatishia usalama wa karibu watoto nusu milioni mjini humo.

Sehemu moja ya taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imesema: "UNICEF imepokea ripoti kwamba watoto, familia na wafanyakazi wa matibabu walikwama hospitalini kwa saa kadhaa, ikiwa ni pamoja na ndani ya Hospitali ya Watoto ya Al Jalaa, wakati wa mapigano. Kwa saa kadhaa, huduma za dharura hazikuweza kufikishwa kituoni hapo. Taarifa zinasema kuwa familia za raia zina huzuni kubwa hasa hofu wanayoonekana nayo watoto  kutokana na ghasia."

Shirika hilo limezitaka pande hasimu kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto ambazo zinawajibisha kulindwa usalama wa watoto na miundombinu wanayoitegemea.

Watoto nusu milioni waingia hatarini kutoka na ghasia mjini Tripoli Libya

 

Mapigano makali yalizuka mwishoni mwa Jumatatu huko Tripoli kati ya vikosi vinavyomtii Waziri Mkuu Abdul-Hamed Dbeibah, ikiwa ni pamoja na Brigedi ya 444, na kundi lenye nguvu la wanamgambo wenye uhusiano na Baraza la SSA baada ya kuenea taarifa za kuuawa mkuu wa SSA, Abdul Ghani al-Kikli, anayejulikana kwa jina maarufu la "Ghaniwa."

Huku hayo yakiripotiwa, jana Alkhamisi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei alielezea wasiwasi wake kuhusu mapigano makali yanayoendelea kati ya makundi yenye silaha kwenye mji mkuu wa Libya Tripoli, akitaka kusitishwa mara moja ghasia na umwagaji damu. Alisema hayo huku kukiwa na ripoti za kuendelea mapigano kati ya makundi hayo mawili hasimu mjini Tripoli.