Iran kuishtaki "Google" kwa kupotosha jina la "Ghuba ya Uajemi"
Kituo cha Kitaifa cha Anga za Juu cha Iran kimesema kitachukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Google ya Marekani na majukwaa mengine ya kimataifa kutokana na kupotoshwa kwa jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi.
Hossein Dalirian, msemaji wa kituo hicho amesema kuwa, suala hilo litafuatiliwa kupitia njia za kisheria za kimataifa, akieleza kuwa huo ni upotoshaji wa makusudi wa ukweli uliothibitishwa wa kijiografia na kihistoria.
Amesema matumizi ya hivi majuzi ya majina yaliyobuniwa badala ya Ghuba ya Uajemi katika baadhi ya majukwaa ikiwemo Google, yameibua hisia kali kutoka kwa jamii wa Iran na hata baadhi ya shakhsia wa kimataifa.
Dalirian amesisitiza kwamba, "Ghuba ya Uajemi" imekuwa ikitumika mara kwa mara kwa maelfu ya miaka katika hati za kihistoria, ramani, na mikataba, na kutambuliwa na taasisi zenye mamlaka kama vile Kundi la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Majina ya Kijiografia chini ya Azimio 715 la ECOSOC la Umoja wa Mataifa.
Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaona matumizi ya majina bandia kuwa ukiukaji wa utambulisho wake wa kitaifa na ukiukaji wa Kifungu cha 19(3) cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa. Viongozi wa Iran wanasisitiza kuwa, Ghuba hii imekuwa Ghuba ya Uajemi kwa miaka na mikaka, na daima itasalia kuwa Ghuba ya Uajemi."
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi alitahadharisha kuhusu ghadhabu za Wairani wote baada ya kuripotiwa kwamba, yumkini Trump akabadili jina la Ghuba ya Uajemi katika ziara yake ya wiki hii katika eneo hili.
Si vibaya kuashiria hapa kuwa, mapema mwaka huu, Mexico ilijibu pia madai ya Rais Donald Trump wa Marekani na kumwambia wazi kwamba, jina la Ghuba ya Mexico kamwe halitobadilika na kuwa "Ghuba ya Amerika."