NATO inayoongozwa na Marekani yakumbwa na sakata la ufisadi
(last modified Fri, 16 May 2025 06:48:39 GMT )
May 16, 2025 06:48 UTC
  • NATO inayoongozwa na Marekani yakumbwa na sakata la ufisadi

Imefichuka kuwa, nchi nyingi duniani zimeanzisha uchunguzi wa rushwa katika mfumo wa ununuzi wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) linaloongozwa na Marekani.

Polisi wamefanya kamata kamata na misako katika nchi kadhaa kama sehemu ya uchunguzi wa ufisadi kwa wafanyikazi wa sasa na wa zamani wa Wakala wa Msaada na Ununuzi wa NATO (NSPA).

Russia Today imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, misako hiyo, iliyoratibiwa na Eurojust - wakala wa jinai wa EU - imefanyika huko Luxembourg, Ubelgiji, Uholanzi, Uhispania, Italia na Marekani. Muungano huo wa kijeshi wa Magharibi uliliambia gazeti la Luxembourg Times Jumatano kwamba, makao makuu ya NSPA huko Grand Duchy, yalikuwa tayari yameanzisha uchunguzi huo.

"NATO - ikiwa ni pamoja na NSPA - inafanya kazi kwa karibu na utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha kuwa wahalifu wanafikishwa mahakamani," msemaji wa muungano huo, Allison Hart amesema. 

Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte aliwaambia waandishi wa habari mjini Ankara jana Alkhamisi kwamba, kambi hiyo ya kijeshi inafanya kazi na mamlaka husika. "Tunataka kujua mzizi wa (sakata) hili," Rutte alisema. Uchunguzi huo unafanyika huku wanachama wa NATO wakitafuta njia za kuimarisha ulinzi wao wenyewe na kuzalisha silaha zaidi zitakazopelekwa Ukraine.

Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kwa miaka mingi sasa limekuwa likikumbwa na tuhuma za uhalifu na kashfa za ufisadi. Hivi karibuni, Alfred Dozias, mtaalamu wa zamani wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa alisema analitazama shirika hilo kuwa ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa binadamu duniani.