Wakuu wa ujasusi watembelea Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance. Kulikoni?
Katika hatua ya kwanza ya aina yake, wakuu wa mashirika ya ujasusi na usalama kutoka nchi za Afrika Mashariki wametembelea Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) magharibi mwa Ethiopia.
Ziara hiyo ilifanyika jana Jumatano kando ya mkutano wa kikanda mjini Addis Ababa uliowakutanisha pamoja wakuu 13 wa mashirika ya ujasusi na usalama kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Maafisa hao walipewa taarifa kuhusiana na maendeleo ya ujenzi na uendeshaji wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD), na kusikiliza maelezo ya kina ya uwezo wa kiufundi na uzalishaji wa mradi huo.
Naibu Mkurugenzi wa Bwawa la Renaissance, Mhandisi Ephraim Haile-Mekel, amesema kuwa bwawa hilo sasa limekamilika kimuundo na limeingia katika awamu halisi ya uzalishaji, kwa sasa linazalisha takriban megawati 1,800 za umeme. Amesema anatarajia uwezo wa uzalishaji kuongezeka hadi megawati 2,600 ndani ya miezi mitatu ijayo.
Amesema kuwa ziwa la bwawa hilo limejaa kabisa, na kutengeneza hifadhi ya kimkakati ya maji ambayo ameitaja kuwa ni "benki ya maji" ambayo inaweza kutegemewa kufidia upungufu wowote wa maji wakati wa ukame.
Malengo ya Ziara:
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Huduma ya Usalama wa Taifa ya Ethiopia, Tazer Gebregziabher, amesema kuwa ziara ya wakuu wa vyombo vya usalama na ujasusi barani Afrika kwenye Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) inakuja kama sehemu ya juhudi za serikali ya Addis Abab za kuweka wazi ukweli kuhusiana na mradi huo na kukanusha kile alichokiita uvumi na kampeni za kupotosha za vyombo vya habari.
Ameeleza kuwa ziara hiyo imekuja wakati muhimu, huku mradi wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance ukikaribia hatua za mwisho za kukamilika na kuwa hali halisi jiografia ya kisiasa yenye taathira katika eneo hilo.
Amesisitiza kuwa mradi huo ni ushahidi wa kivitendo wa uwezo wa nchi za Afrika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
Ujenzi wa bwawa hilo umeibua mvutano mkubwa wa maji kati ya nchi Ethiopia, Misri na Sudan tangu mwaka 2011 hadi sasa.
Misri na Sudan zinahofia kwamba bwawa hilo kubwa lililogharimu dola bilioni 4.2 litapunguza kwa kiasi kikubwa sehemu ya maji ya Mto Nile wanayopokea, na mara kadhaa zimeiomba Addis Ababa isitishe kulijaza hadi makubaliano yafikiwe.