Pezeshkian amjibu Trump: Inaonekana huwajui kabisa Wairani
(last modified Thu, 15 May 2025 07:39:27 GMT )
May 15, 2025 07:39 UTC
  • Pezeshkian amjibu Trump: Inaonekana huwajui kabisa Wairani

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amejibu kauli za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Iran na kusema kuwa, inaonekiana kiongozi huyo wa Marekani hawafahamu wananchi wa Iran.

Rais Pezeshkian amesema hayo wakati wa mkutano wake na wasomi, wenye vipawa na wanaharakati wa uga wa kiutamaduni katika Mkoa wa Kermanshah na kueleza kwamba: "Alichosema Trump kinaonyesha kuwa hawafahamu watu wa Iran, na haelewi chochote kuhusu ghera, uungwana na kujitolea kwao, na anatoa shutuma kwamba Iran ni chanzo cha machafuko na hatari."

Aliongeza: "katika hali ambayo zaidi ya raia 60,000 wasio na hatia wameuawa shahidi huko Gaza, wakiwemo wanawake na watoto, nani alifunga njia zao za kuwafikia chakula, maji na dawa?! Wanasema wana mabomu yasiyofikirika, halafu wanatutuhumu sisi kuwa tunapigia debe vita na umwagaji damu! Je, ni nani anayezipa silaha nchi za eneo hilo na kuzisukuma kuelekea kwenye mifarakano?" nani anayepanda mbege ya fitina, amehoji Rais wa Iran.

Rais wa Iran aliendelea kusema: "madola ya Magharibi yanapigia debe amani mdomoni tu,  lakini kwa miaka 47 yamekuwa yakifanya kila yawezalo kuwapigisha magoti watu wa Iran na utawala wao, na hayajafanikiwa, na hayatafanikiwa kamwe."

Pezeshkian pia amesema: "Wanadai kuwa walilishinda kundi la kigaidi la Daesh, lakini ni nani aliyemuua shahidi Qassim Soleimani, mtu aliyepambana na Daesh?! Ninyi ndio mliowafunza na kuwapa silaha  Daesh, wakati Qassim Soleimani na wenzake ndio waliowaondoa magaidi hawa katika eneo hili."

Pezeshkian alimalizia kwa kubainisha msimamo wa Iran: "Watake amani au la, tutaijenga nchi hii na kuiendeleza kwa nguvu. Sisi ni watetezi wa amani, si watetezi wa vita, lakini heshima na fahari yetu haviuzwi, na hatutapiga magoti mbele ya nguvu yoyote, wala hatutasalimu amri."