Umeme wakatika kikamilifu Khartoum kutokana na mashambulizi ya droni za RSF
(last modified Fri, 16 May 2025 10:18:39 GMT )
May 16, 2025 10:18 UTC
  • Umeme wakatika kikamilifu Khartoum kutokana na mashambulizi ya droni za RSF

Shirika la Umeme la Sudan alisema kuwa, vituo viwili vya kuzalisha umeme vimeshambliwa kwa droni (ndege zisizo na rubani) za Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na kusababisha kuwaka moto na kukatika umeme katika mji mkuu.

Taarifa ya shirika hilo imesema: "Ndege zisizo na rubani za wanamgambo zimeshambulia kituo kidogo cha Al-Markhiat na kituo cha usambazaji umeme katika jiji la Omdurman."

Limesema: "Shambulio hilo limesababisha kukatika umeme katika maeneo yote ya Khartoum, na kuzidisha mateso ya raia na usumbufu wa kupata huduma."

"Vikosi vya Ulinzi wa Raia vinafanya juhudi kubwa kuzima moto huo. Tathmini ya kiufundi ya uharibifu uliosababishwa na mashambulio hayo itafanywa baadaye, ikifuatiwa na hatua muhimu za matengenezo," imeongeza taarifa hiyo.

Tangu tarehe 15 Aprili 2023, RSF imekuwa ikipambana na jeshi la Sudan SAF kwa ajili ya kuidhibiti nchi hiyo. Hadi hivi sasa mapigano hayo ya uchu wa madaraka kati ya majenerali wa kijeshi yameshapelekea maelfu ya watu kuuwa na kuigeuza Sudan kuwa nchi yenye moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa na taarifa za tawala za kieneo na serikali za mitaa, zaidi ya watu 20,000 wameshauawa na milioni 15 wamekimbia makazi yao nchini Sudan.

Lakini uchunguzi wa duru za kimataifa umekuja na takwimu za kutisha. Uchunguzi huo uliofanywa na taasisi za Marekani unasema kuwa idadi ya watu waliouwa nchini Sudan kutokana na vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe ni karibu watu 130,000.