Faida za makubaliano ya Iran na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia
(last modified Sat, 17 May 2025 12:00:47 GMT )
May 17, 2025 12:00 UTC
  • Faida za makubaliano ya Iran na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia

Ali Ahmadnia, Mkuu wa Masuala ya Habari wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa takriban asilimia 87 ya bidhaa zinazouzwa kati ya Iran na nchi tano wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU) zitauzwa kati ya nchi hizo bila kutozwa ushuru.

Amesema: "Kulingana na makubaliano hayo, takriban asilimia 87 ya bidhaa zinazouzwa kati ya Iran na nchi tano wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU), ambazo ni Russia, Kazakhstan, Belarus, Armenia na Kyrgyzstan hazitatozwa ushuru kuanzia Mei 15." Kwa mujibu wa Makubaliano ya Biashara Huria ya Umoja wa Eurasia na Iran, kiwango cha biashara baina ya Iran na nchi hizo tano kinatarajiwa kuongezeka na kufikia kwa uchache dola bilioni 10.

Malengo na vipaumbele vya Umoja wa Forodha wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia yametangazwa kuwa ni pamoja na kuondolewa ushuru wa forodha wa ndani ya nchi wanachama, kubuniwa ushuru wa pamoja wa nje na kupanuliwa soko la pamoja kati ya nchi wanachama. Lengo la umoja huu ni kuunda mazingira mamoja ya kiuchumi, kukuza soko la pamoja na kufikia usafirishaji huru wa bidhaa na mitaji, kupunguza bei za bidhaa kwa kupunguza gharama za usafirishaji wa malighafi, kuimarisha ushindani unaofaa katika soko la pamoja, na kutekeleza sera za pamoja katika sekta ya kilimo, nishati, teknolojia na usafirishaji.

Hivi sasa, wanachama wa umoja huu ni Russia, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan na Armenia, ambazo pia ni wanachama wa Jumuiya ya Forodha ya Eurasian. Iran, Tajikistan, Georgia, Uzbekistan, Moldova, Ukrainia, Pakistani, Uturuki, Uchina na Vietnam pia ni machaguo mengine yanayoweza kuwa wanachama katika Umoja huu wa Eurasia.

Ni wazi kuwa kuondolewa ushuru kwa bidhaa za Iran na Jumuiya ya Eurasia kutakuwa na matokeo chanya kwa uchumi wa Iran. Soko la watu milioni 180 la Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia ni hatua ya kistratijia itakayosaidia katika utungaji wa sera za kiuchumi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa taifa na kupunguza utegemezi kwa masoko ya nchi za Magharibi hususan katika muktadha wa vikwazo dhidi ya Iran vinavyotekelezwa na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.

Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU) Iran

Kuongezeka kiwango cha biashara kati ya Iran na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia pia kumeongeza sehemu ya malipo ya biashara kwa kutumia fedha za kitaifa hadi asilimia 70, jambo ambalo linaweza kurahisisha miamala ya kifedha ya Iran na kupunguza utegemezi kwa mfumo wa kifedha wa Magharibi katika mazingira ya vikwazo.

Kupanuliwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na umoja huu kunaweza kusaidia kuendeleza miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi wa bidhaa na hivyo kuiletea nchi mapato makubwa ya fedha za kigeni. Pia, miradi kama vile Ukanda wa Kaskazini-Kusini na Mpango wa Ukanda na Barabara wa China (ufufuliwaji wa Njia ya Hariri) inaweza kuwa na nafasi muhimu katika suala hili.

Ukanda wa Kaskazini-Kusini unajumuisha njia mbili za nchi kavu na reli mashariki na magharibi mwa Bahari ya Caspian, pamoja na njia mseto ya pamoja ya bahari na ardhi ambayo inajumuisha Russia na Iran.

Kwa kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na gesi, Iran ni mshirika muhimu katika kuhakikisha usalama wa nishati kwa nchi wanachama wa Umoja wa Eurasia, hasa Armenia na Belarus. Pia, uanachama huu unaweza kufungua njia ya kuhamishwa teknolojia na uwekezaji wa pamoja katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na magari, petrokemikali na utalii.

Ushirikiano wa Iran na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia pia unaimarisha uwepo wa Iran katika eneo la Asia Magharibi, jambo ambalo linaweza kupelekea kuimarika uthabiti wa kisiasa na usalama katika eneo hili. Ushirikiano huu unatoa fursa mpya za kiuchumi, na unaweza kutumika kama chombo cha kupunguza mashinikizo ya vikwazo na kuimarisha nafasi ya kimkakati ya taifa hili katika ngazi za kikanda na kimataifa.

Mchakato wa kuweka malengo na mipango ya kiuchumi katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utaharakishwa kupitia makubaliano mapya na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia. Ushirikiano kati ya Iran na wanachama wa umoja huu utakuwa na matokeo chanya ya kiuchumi kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano na kuongeza biashara katika eneo.

Kutotozwa ushuru kwa asilimia 87 bidhaa za Iran na nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Eurasia ni hatua muhimu na yenye taathira kubwa katika mustakabali wa ushirikiano wa kiuchumi katika eneo la Asia ya Kati na  Eurasia. Uwezo wa nchi wanachama wa umoja huu na Iran pia utaweka msingi unaofaa kwa ajili ya ustawi wa biashara, kubadilishana bidhaa na ushirikiano kwa ajili ya uwekezaji wa kiuchumi wa pande mbili.