Hofu ya kukamatwa yamfanya Netanyahu afute safari yake ya Vatican
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amefuta safari yake ya Vatican akihofia kutekelezwa waranti wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC unaotaka atiwe mbaroni kwa kutenda jinai za kivita Palestina.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ofisi yake iliamua kufuta safari hiyo baada ya kufanya mawasiliano na viongozi wa Italia na Vatican.
Gazeti la Kizayuni la "Yediot Aharonot", linalochapishwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, liliandika Ijumaa usiku, likieleza kufutwa safari hiyo ya Netanyahu, kwamba alikuwa na nia ya kuhudhuria kuapishwa Papa mpya huko Vatican, lakini ameghairi safari hiyo kutokana na wasiwasi wa uwezekano wa kutekelezwa kwa hati ya kukamatwa kwake iliyotolewa dhidi yake.
Novemba mwaka jana (2024), Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa hati za kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant aliyekuwa waziri wake wa vita baada ya kuwafungulia mashtaka ya kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza, ambako utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kinyama na kufanya mauaji ya kimbarii tangu mwezi wa Oktoba mwaka jana.
Hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ya kutoa waranti ya kukamatwa Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant, Waziri Mkuu na waziri wa zamani wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel iliakisiwa pakubwa kimataifa kwa kutilia maanani umuhimu wake na pia kutokana na kutochukuliwa hatua kama hiyo huko nyuma dhidi ya viongozi wa utawala huo ghasibu.