Togo yathibitisha kesi ya kwanza ya ugonjwa wa Mpox
(last modified Sat, 17 May 2025 11:00:08 GMT )
May 17, 2025 11:00 UTC
  • Togo yathibitisha kesi ya kwanza ya ugonjwa wa Mpox

Togo imethibitisha kesi ya kwanza ya Mpox nchini humo, Wizara ya Afya na Usafi wa Umma ya nchi hiyo imetangaza katika taarifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya jana Ijumaa, kisa hicho kiligunduliwa na kuthibitishwa jana Ijumaa, na mgonjwa huyo ni mwanamke mwenye umri wa miaka 22 anayeishi katika mji mkuu wa Lome. Kwa sasa anapokea matibabu katika kitengo cha magonjwa ya kuambukiza.

Katika kukabiliana na hali hii, wizara imesema imechukua hatua za kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, onyo la mapema, uthibitisho wa kesi, udhibiti wa kesi zilizogunduliwa, na kampeni za uhamasishaji wa umma juu ya hatua za kinga.

Haya yanajiri huku eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, likikabiliwa na hali mbaya katika mapambano yake dhidi ya mripuko wa ugonjwa wa Mpox. 

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika kilisema karibuni kuwa, wagonjwa wa Mpox zaidi ya 600 wametoroka katika hospitali mbalimbali kufuatia kushtadi mapigano ya waasi wa M23. 

Aidha mapema mwaka huu, Kenya ilithibitisha kuwepo wagonjwa wengine 2 wenye maambukizi ya Mpox na hivyo kufanya jumla ya kesi za ugonjwa huo zilizothibitishwa hadi sasa nchini humo kufikia 33.

Hivi karibuni, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitahadharisha kuwa virusi vya Mpox aina ya Clade 1b ambayo vinaendelea kuenea kwa kasi katika sehemu mbali mbali duniani.

Barani Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inasalia kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi, na hadi sasa inaongoza kwa idadi kubwa ya maambukizi yaani watu 49,000.  Ugonjwa huo wa Mpox umeuwa watu 1,100 katika bara la Afrika tangu Januari mwaka jana.