Iran: Israel iliundwa kwa damu; mauaji ya kimbari lazima yakomeshwe sasa
(last modified Fri, 16 May 2025 07:22:19 GMT )
May 16, 2025 07:22 UTC
  • Iran: Israel iliundwa kwa damu; mauaji ya kimbari lazima yakomeshwe sasa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa kwa mnasaba wa Siku ya Nakba na kusema kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel "uliasisiwa katika msingi wa umwagaji damu" na kwamba jamii ya kimataifa ina wajibu wa kukomesha mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza.

Tamko hilo lililotolewa jana Alkhamisi, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya maangamizi ya kizazi cha wananchi madhulumu wa Palestina katika tukio la Siku ya Nakba mnamo Mei 15, 1948.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Siku ya Nakba ulikuwa mwanzo wa kampeni ya miaka 80 ya ukoloni wa kuwafuta kabisa wananchi wa Palestina.

Imesema utawala wa Israel umekuwa ukifanya jinai za kivita na mauaji ya halaiki bila ya kuadhibiwa, huku ukiungwa mkono na madola ya Magharibi. Tehran imetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za kisheria  viongozi wa Israel kwenye vyombo vya sheria vya kimataifa.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema, utawala wa Israel umekuwa ukifanya ukatili wa miongo kadhaa, ikiwemo kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kwenye makazi yao, kuwataabisha kwa njaa,  na kufanya mauaji ya umati hususan dhidi ya wanawake na watoto.

Taarifa hiyo imeitaja Washington kuwa "mshirika (wa Israel) katika mauaji ya halaiki," ikiilaumu kwa kuuikinga kifua utawala huo ili usiwajibishwe katika Umoja wa Mataifa na mahakama za kimataifa.

Tehran imezitaka nchi zote duniani kutimiza wajibu wao wa kisheria na kimaadili chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mikataba ya Geneva kwa kukomesha umwagaji damu huo wa Wazayuni.