Zakzaky: Mashambulizi ya kigaidi ya Israel yanapasa kulaaniwa duniani kote
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria (IMN), Sheikh Ibrahim Zakzaky amelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran na kuelezea hujuma hizo za utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi huru kuwa ni kitendo cha juu zaidi cha uchokozi, kinachopaswa kulaaniwa duniani kote.
Amesema kuwa, utawala haramu na ghushi wa Israel umetekeleza mashambulizi hayo kwa ridhaa na baraka kamili za serikali ya Marekani. Sheikh Zakzay amelaani vikali mashambulio hayo ambayo yamelenga raia wasio na hatia kwa makusudi.
Mwanachuoni huyo mashuhuri wa Nigeria ameeleza bayana kuwa: "Kitendo hiki cha kichokozi hakijawahi kuonekana tena hapo awali. Ni ukatili. Ni kitendo cha uchokozi. Ni ukiukaji wa kila haki unaopaswa kulaaniwa na kila mtu mwenye fikra sahihi duniani kote."
Kiongozi huyo wa Kiislamu nchini Nigeria amesisitiza juu ya uungaji mkono wao kwa wananchi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameeleza kuwa, "Tunaiunga mkono Iran"
Wakati huo huo, mamia ya Waislamu walikusanyika na kuandamana katika mitaa ya mji wa Kano, kaskazini mwa Nigeria kulaani mashambulizi hayo ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kueleza mshikamano na watu wa Iran, pamoja na Wapalestina ambao wamekuwa wakikabiliwa na hujuma za mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Kadhalika wamepongeza jibu la haraka la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni, wakisema kwamba Israel lazima itiwe adabu kwa jinai zake.
Kabla ya hapo, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilikosoa mienendo ya serikali za Magharibi na kuitaja kuwa ya kinafiki kuhusiana na jibu la Iran kwa Israel. Taarifa ya harakati hiyo imesema kuwa, "Iran ina kila haki ya kujilinda. Kinachoshangaza ni unafiki wa serikali za Magharibi. Serikali hizi za Magharibi, baada ya kuona Iran imechukua hatua ya kulipiza kisasi, sasa zinatoa mwito wa kujizuia, na kuzitaka pande zote mbili kuchukua hatua za kujizuia.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema shambulio la Israel dhidi ya Iran, ambalo lilisababisha kuuawa shahidi maafisa kadhaa wakuu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia, linapasa kulaaniwa vikali na halipaswi kuvumiliwa. IMN imesema Marekani inahusika katika mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya Iran, licha ya taarifa ya Rais Donald Trump kudai Marekani haikuhusika.