Umuhimu wa Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran
Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran unafanyika kwa kuwashirikisha takriban wageni 200 kutoka nchi 53 duniani. Mkutano huo umefunguliwa rasmi mapema leo katika hafla iliyohudhuriwa na Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araqchi.
Mkutano wa Kimataifa wa Tehran Dialogue Forum unafanyika leo Jumapili na kesho Jumatatu, Mei 18 na 19, 2025 ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi. Wageni 200 kutoka nchi 53 duniani wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa nchi mbalimbali pia wanashiriki katika mkutano huo.

Miongoni mwa washiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran ni wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, jumbe kutoka nchi za Amerika ya Kaskazini, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Uturuki, Armenia, India, Japan, China, Russia, Saudi Arabia, Iraq na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, Mawaziri wa Mambo ya Nje, wawakilishi maalumu wa serikali.
Mojawapo ya taasisi zinazotambulika kimataifa ambazo zinashiriki katika kongamano hili la Tehran ni Taasisi ya Aguash, ambayo inashiriki inajishughulisha na utafiti wa upokonyaji silaha katika nyanja ya kimataifa.
Hali ya sasa ya Palestina, Muqawama, matukio yanayoendelea kushuhudiwa sasa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, utaratibu mpya wa eneo la Asia Magharibi na miundo mbadala ya mfumo wa kimataifa ni mada zinazojadiliwa na kuchunguzwa katika Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran.
Amir Khan Mottaqi, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan, Nechirvan Barzani, Rais wa Eneo la Kurdistan la Iraq, na Armen Grigoryan, Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Armenia, pamoja na Sirojiddin Muhriddin Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Tajikistan, ni miongoni mwa maafisa wanaoshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran.

Kongamano la Kimataifa la Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran ni tukio la kidiplomasia na kiutamaduni ambalo linalenga kuimarisha mazungumzo kati ya nchi na staarabu mbalimbali hususan katika Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa Kiislamu. Jukwaa hili pia linatumika kama sehemu ya kubadilishana mawazo kati ya nchi na tamaduni mbalimbali, na huchukua hatua za kupunguza mivutano na kuzidisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatumia mkutano huu kueleza misimamo yake katika nyanja za kisiasa, kiusalama na kiutamaduni, na kuwasilisha maoni na vipaumbele vyake katika uga wa siasa za nje kuhusu masuala ya kimataifa. Moja ya mada kuu za mkutano huu ni kutilia mkazo mshikamano wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kukabiliana na changamoto kama vile misimamo mikali, vikwazo na uingiliaji kati wa mataifa ajinabi.
Matukio ya Asia Magharibi, Palestina, Yemen, na uhusiano kati ya nchi za Kiislamu ni miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika mkutano huu. Tukio hili litaisaidia Iran kuimarisha taswira yake kama nchi inayounga mkono mazungumzo na amani ya kimataifa na kukabiliana na propaganda hasi za Magharibi.
Mkutano wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran pia una nafasi muhimu katika diplomasia ya pande kadhaa ya Iran na unatumika kama stratijia ya kidiplomasia ya kupanua uhusiano wa kiutamaduni na kisiasa na nchi nyingine hususan katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tukio hili pia linadhihirisha jitihada za Iran za kusimamia suala la kukurubisha pamoja mitazamo ya Kiislamu na kukabiliana na sera zinazozusha migawanyiko.
Kufanyika Mkutano wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran na kukaribishwa pakubwa mkutano huu na viongozi wa kanda hii pamoja na shakhsia wenye ushawishi na taasisi huru za kimataifa, kunaonyesha nafasi athirifu na chanya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika matukio ya kieneo na kimataifa.
Kongamano la Jukwaa la Mazungumzo la Tehran pia linabainisha umuhimu wa nafasi ya Iran kama daraja la mawasiliano na kidiplomasia katika eneo la Magharibi mwa Asia na litadhamini mwelekeo wenye mafanikio wa sera za nje za Iran katika kupanua ushirikiano na nchi za eneo hilo.