Wanamichezo 560 wameuawa na Israel katika vita vya Gaza
(last modified Sun, 18 May 2025 10:54:32 GMT )
May 18, 2025 10:54 UTC
  • Wanamichezo 560 wameuawa na Israel katika vita vya Gaza

Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Michezo wa Palestina, ametangaza kuuawa shahidi kwa wanariadha 560 wa Kipalestina na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya michezo katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza hujuma ya kinyama ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023.

Muntaser Adkaydek, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Michezo wa Palestina, amesema hayo katika katika Kongamano la AIPS huko Rabat, Morocco na kuongeza kuwa, kulenga wanariadha na miundombinu ya michezo kunatishia mustakabali wa michezo ya Palestina, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kukomesha mashambulizi haya.

Aidha ametangaza kuzinduliwa mpango wa "Waandishi wa Habari wa Matumaini" na Kamati ya Vyombo vya Habari vya Michezo ya Palestina, kwa ushirikiano na vyombo vya habari vya Kiarabu na kimataifa, kusaidia vijana wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, na kusema: "Uwezeshaji wa kiuchumi, msaada wa kisaikolojia, kuimarisha sauti ya watu wa Palestina katika Ukanda huo, na malengo ya kibinadamu ya kuanzishwa kwa michezo ni miongoni mwa malengo ya kuanzishwa waandishi wa matumaini ya michezo."

Hata hivyo baadhi ya duru za Palestina zinasema kuwa, idadi ya wanamichezo wa Kiipalestina waliouawa tangu Israel ianzishe mashambulio yake ya kinyama huko Palestina inapindukia 700.

Mustafa Sayam, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyombo vya Habari vya Michezo vya Palestina ametangaza kuwa, wanamichezo 708 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika vita vya Gaza.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hivi karibuni pia Shirikisho la Soka la Palestina lilitangaza kuwa, mamia ya wanamichezo wameuawa shahidi tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha hujuma na mashambulio ya kinyama dhidi ya Gaza Oktoba 2023.