WFP yasimamisha usambazaji wa chakula Darfur Kaskazini, Sudan
(last modified Sat, 01 Mar 2025 07:14:39 GMT )
Mar 01, 2025 07:14 UTC
  • WFP yasimamisha usambazaji wa chakula Darfur Kaskazini, Sudan

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesitisha usambazaji wa chakula cha msaada katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam nchini Sudan kutokana na kushtadi mapigano kati ya jeshi la serikali na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Leni Kinzli, Msemaji wa WFP nchini Sudan, wakati wa mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva jana Ijumaa alisema: Mapigano makali katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam, eneo la Darfur Kaskazini, yameilazimu WFP kusitisha kwa muda ugawaji wa chakula na lishe kwa watu waliokimbia makazi yao.

Ameonya kwamba, ikiwa hakuna msaada wa haraka utatolewa, maelfu ya familia zilizokata tamaa huko Zamzam watakufa kwa njaa katika wiki zijazo. Kinzli amesisitiza umuhimu wa kurejesha shughuli ya utoaji salama na kwa wakati msaada wa kuokoa maisha, akisema: "Kwa ajili hiyo, mapigano lazima yakome, na mashirika ya kibinadamu lazima yapewe dhamana ya usalama."

Ametahadharisha kuwa, watu milioni mbili katika maeneo 27 kote Sudan kwa sasa wanakumbwa na njaa au wako katika hatari ya kufa njaa.

Wanamgambo wa RSF

Kabla ya hapo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk alionya juu ya hatari ya kuongezeka zaidi kwa vita nchini Sudan na kusema kwamba, kuna hatari kubwa ya kutokea vifo kutokana na njaa kwa kiwango cha kuogofya.

Tangu kuzuka vita vya ndani huko Sudan mwaka 2023 kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, karibu watu milioni 8.8 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi hiyo huku milioni 3.5 wakikimbilia nchi jirani.