Wapalestina 70 wauawa shahidi katika mashambulio ya kinyama ya Israel Ghaza
(last modified Tue, 05 Nov 2024 12:52:38 GMT )
Nov 05, 2024 12:52 UTC
  • Wapalestina 70 wauawa shahidi katika mashambulio ya kinyama ya Israel Ghaza

Wapalestina wasiopungua 70 wameuawa shahidi na makumi ya wengine wamejeruhiwa, akthari yao wakiwa ni wa sehemu ya kaskazini ya Ukanda wa Ghaza katika mashambulizi ya kinyama ya anga na ardhini yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hilo ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.

Shirika rasmi la habari la Palestina Wafa, likiwanukuu maafisa wa huduma za tiba na vyanzo vya ndani limeripoti kuwa watu wasiopungua 20 walipoteza maisha katika shambulio la anga lililolenga nyumba moja katika mji wa kaskazini uliozingirwa wa Beit Lahiya.
 
Watu wengine wanne waliuawa shahidi na wengine kadhaa walijeruhiwa wakati ndege za kivita za jeshi la Israel ziliporipua nyumba moja katika kitongoji cha Tuffah katika mji wa Ghaza kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.
 
Vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni vimeshambulia pia kwa mabomu mahema ya Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao katika eneo la az-Zawayda katikati mwa Ghaza.
 
Kwa mujibu wa Wafa, watu sita, ikiwa ni pamoja na watoto wawili - mmoja mwenye umri wa miaka sita na mwingine mwenye umri wa miaka minne-, waliuawa shahidi katika shambulio hilo, huku idadi kamili ya waliojeruhiwa ikiwa haijulikani.
Wapalestina wanaoendelea kuuawa shahidi kila uchao kwa mashambulio ya Israel dhidi ya Ghaza

Mama wa mmoja wa watu waliouawa amesema, watu hao walichomwa moto katika shambulio hilo wakiwa wamelala.

 
Shambulio hilo lilikuwa la tatu kufanywa na jeshi katili la utawala haramu wa Israel dhidi ya mahema ya watu waliohamishwa katika masaa ya hivi karibuni, kufuatia mashambulio dhidi ya miji ya Deir el-Balah na Khan Yunis, yaliyosababisha vifo vya watu watano.

Wakati huohuo, Wizara ya Afya ya Ghaza imetangaza kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni "wanaendelea kushambulia na kuharibu" Hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa ukanda huo, na kusisitiza kuwa Israel inapanga "kuwaua" wafanyakazi wa huduma za tiba wanaokataa kuondoka hospitalini hapo.

Eid Sabbah, Mkurugenzi wa uuguzi wa hospitali hiyo amesema, watoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na watoto wachanga waliowekwa kwenye vifaa vya uangalizi (incubators), ni "waathirika wa moja kwa moja" wa mashambulizi yanayofanywa na jeshi la Israel kwenye hospitali hiyo.../