Mar 30, 2024 07:21 UTC
  • Shirika la kimataifa la usalama wa chakula: Sudan inahitaji hatua za haraka kukabiliana na njaa

Shirika la usalama wa chakula duniani linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa (IPC) lilionya jana Ijumaa kuhusu haja ya kuchukuliwa hatua za haraka "kuzuia kushamiri vifo, kuporomoka kabisa kwa njia za kujipatia riziki na kuepusha janga la njaa nchini Sudan."

IPC imesema imepitia ushahidi wa karibuni na kuchapisha onyo jana ili "kuelezea wasiwasi wake mkubwa" kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya nchini Sudan na kushinikiza kuchukuliwa hatua za haraka "kuzuia baa la njaa".

Ripoti ya IPC imesema: "Bila ya kusitishwa mara moja kwa mapigano na kupelekwa msaada mkubwa ya kibinadamu, wakazi wa Khartoum, Gezira, Darfur Kubwa, na Jimbo kuu la Kordofan wako katika hatari ya kufikia viwango vibaya zaidi vya ukosefu wa usalama chakula na utapiamlo katika msimu ujao wa kiangazi, ambao utaanza Aprili 2024.”

Tathmini hii ilipangwa kutolewa Desemba mwaka jana, na ilihitimisha kuwa karibu watu milioni 5 wanakabiliwa na utapiamlo mkali, ikiwa ni pamoja na watoto milioni 3.6 chini ya umri wa miaka mitano, na wanawake milioni 1.2 wajawazito na wanaonyonyesha.

IPC: Wanawake milioni 1.2 wajawazito na wanaonyonyesha wanakabiliwa na utapiamlo nchini Sudan.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi huu lilitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Vilevile Umoja wa Mataifa umezitaka pande zinazozozana Sudan kuweka chini silaha na kuwalinda raia hasa wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Takwimu za UN zinaonesha kuwa, mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na Kamanda Hamdan Dagalo yameshaua watu karibu 14,000 hadi sasa, na kupelekea mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan huku watu milioni 25 wakihitaji misaada ya dharura.

Tags