May 01, 2024 10:52 UTC
  • Russia yaruhusu wanawake Waislamu wanaoomba uraia kutumia picha za vazi la Hijabu

Serikali ya Russia imelegeza masharti ya kanuni zinazohusu maombi ya raia wa kigeni wanaoomba uraia, na itaruhusu mwanamke wa Kiislamu kutumia picha za paspoti zinazomuonesha akiwa amevaa vazi la staha la Kiislamu la Hijabu. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo.

Sheria hiyo mpya itaanza kutumika Mei 5, siku kumi baada ya kuchapishwa.
 
Taarifa hiyo imefafanua kwa kusema, "katika hali ambapo imani za kidini za mwombaji hazimruhusu kujitokeza mbele ya maajinabi pasi na kufunika kichwa, zitolewe picha zilizofunika kichwa lakini zisizoziba mviringo wa uso" .
 

Hata hivyo, taarifa hiyo imeongeza kuwa, picha zilizo na mitandio ambayo inaficha kikamilifu au kwa kiasi fulani kidevu cha mwombaji hazitakubaliwa.

Mamlaka za Russia tayari zimewaruhusu raia wake kutumia picha wakiwa wamevalia hijabu wanapotuma maombi ya pasipoti, leseni za udereva, vibali vya kufanyia kazi na hatimiliki.

Biysultan Khamzaev, mjumbe wa Kamati ya Usalama na Kupambana na Ufisadi ya Bunge la nchi hiyo Duma ameliambia gazeti la bunge hilo kwamba, sheria hizo mpya zitawaruhusu waumini kutekeleza mafundisho yao ya kidini, na kuhakikisha pia usalama wa serikali, kwa sababu kama zilivyo data zingine, sura inahitajika ili mifumo ya ufuatiliaji ya video iweze kumtambua mtu.

Mwanamke Muislamu wa Russia aliyevalia vazi la staha la Hijabu

Katika enzi za utawala wa Shirikisho la Kisovieti la Urusi ilikuwa marufuku kuvaa skafu au mtandio wa hijabu katika picha za paspoti.

Lakini baada ya kusambaratika shirikisho hilo mwaka 1991, wanawake Waislamu walianza kutumia picha hizo hadi mwaka 1997, wakati serikali ilipopiga marufuku utaratibu huo. Mnamo mwaka 2003, Mahakama Kuu ya Russia ilitoa hukumu kwamba marufuku hiyo haikuwa halali kisheria.

Marekebisho ya sheria ya paspoti ya mwaka 2021 yanaeleza kuwa watu ambao imani yao haiwaruhusu kuvua vazi linalofunika kichwa kwa sababu za kidini wanaweza kuwasilisha picha zilizofunika kichwa.

Rais Vladimir Putin amesema, Russia ni nchi ya watu wa mataifa na dini kadhaa na inaamiliana na kila mtu kwa heshima, akiongeza kuwa makabila yapatayo 190 yanaishi nchini humo, ambapo baadhi yao yanawakilishwa na mamilioni ya watu".../

 

Tags