Jun 27, 2024 05:50 UTC
  • Kuimarika uhusiano wa Iran na Russia kufuatia kusainiwa mkataba wa usambazaji gesi

Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kutiwa saini mapatano ya kusafirisha gesi ya Russia hadi Iran ni hatua muhimu katika mwelekeo wa kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na hatua athirifu inayolenga kustawisha uchumi wa eneo.

Katika mazunguzo yake ya simu na Rais Vladimir Putin wa Russia siku ya Jumatano, Mohammad Mokhber, Kaimu Rais wa Iran, ameashiria kutiwa saini mapatano ya pamoja ya kusafirisha gesi ya Russia kwenda Iran na kusema kwa kutekelezwa mpango huo, sio tu maslahi ya kiuchumi ya nchi mbili yatadhaminiwa, bali maslahi ya kanda nzima yatapatikana kutokana na mradi huo.

Kuongeza uhusiano wa Iran na Russia kufuatia kusainiwa mkataba wa usambazaji  gesi

Akielezea kuridhishwa kwake na maendeleo ya utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na Moscow, Mokhber amesema uhusiano wa kistratijia wa pande mbili hautabadilika. Amesisitiza umuhimu wa mazungumzo na mtazamo wa pamoja wa Iran na Russia kuhusu masuala ya kieneo, na kuelezea matumaini yake kuwa juhudi za nchi mbili za kuleta utulivu katika eneo, zitazaa matunda yanayotarajiwa.

Kaimu Rais wa Iran pia amelaani shambulizi la kigaidi la hivi karibuni huko Dagestan na kutuma salamu zake za rambirambi kwa serikali na watu wa Russia pamoja na familia za wahanga wa jinai hiyo ya kinyama.

Rais Vladimir Putin, pia ameeleza kuridhishwa kwake na kutiwa saini makubaliano ya pamoja ya kimkakati ya usafirishaji gesi kati ya Russia na Iran, na kuyachukulia makubaliano hayo kuwa tukio muhimu kwa ajili ya kulinda maslahi ya nchi hizi na kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kwa manufaa ya masoko ya eneo na kimataifa.

Rais wa Russia aidha ameridhishwa na ongezeko la kiwango cha biashara kati ya nchi yake na Iran na kusema kubadilishana jumbe za kisiasa ni chaguo bora zaidi la kuweka msingi wa kustawisha uhusiano wa nchi mbili.

Tags