Russia: Hatari ya kutokea vita vya nyuklia inazidi kuongezeka
https://parstoday.ir/sw/news/world-i113372-russia_hatari_ya_kutokea_vita_vya_nyuklia_inazidi_kuongezeka
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametahadharisha kuwa, madola yenye silaha za nyuklia yapo katika hatari ya kuingia katika makabiliano ya moja kwa moja.
(last modified 2024-06-26T11:49:21+00:00 )
Jun 26, 2024 11:49 UTC
  • Russia: Hatari ya kutokea vita vya nyuklia inazidi kuongezeka

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametahadharisha kuwa, madola yenye silaha za nyuklia yapo katika hatari ya kuingia katika makabiliano ya moja kwa moja.

Sergey Ryabkov ameonya kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia duniani katika kikao na wabahari mjini Moscow na kueleza kuwa: Hatari ya kutokea vita baina ya madola yanayomiliki silaha za nyuklia ipo juu.

Amesema nchi za Magharibi zinaendelea kuchochea moto wa kutokea vita vya nyuklia, kwa kuweka masharti magumu na yasiyokubalika kwa ajili ya kufanyika mazungumzo ya usalama.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amebainisha kuwa, "Tumefikia uamuzi kuwa, tunapasa kutafakari kuhusu mustakabali na kupunguza hatari ya kutokea makabiliano ya moja kwa moja. Kwa masikitiko, mahasimu wetu wa Magharibi wametoa masharti magumu ya kufanyika mazungumzo kama hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Ryabkov

Hivi karibuni pia, Rais Vladimir Putin wa Russia alionya kuwa, nchi yake iko tayari kutumia silaha za nyuklia ikiwa kutakuwepo tishio kwa serikali na uhuru wake. Alisema, "Mifumo yetu ya nyuklia ni ya kisasa zaidi kuliko mingine yoyote. Ni sisi tu na Marekani ambao tuna mifumo kama hii. Lakini mifumo yetu ni ya kisasa zaidi."

Aidha, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa karibuni alionya kuhusu dunia kuingia katika mashindano mapya ya silaha za nyuklia ambayo yanaweza kueneza maafa duniani kote. Alisema, "wakati huu ambapo baadhi ya nchi zinatishia kutumia silaha za nyuklia, kivuli cha vita vya nyuklia kinaonekana tena kwenye sayari ya dunia."