Jul 01, 2024 07:18 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Julai Mosi

Natumai u bukheri wa afya msikilizaji mpendwa hapo ulipo. Karibu katika dakika hizi chache za kuangazia kwa ufupi baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa.

Mieleka: Iran bingwa wa Asia

Timu ya mieleka mtindo wa kujiachia (freestyle) ya Iran imeibuka kidedea katika Mashindano ya Ubingwa wa Asia ya mwaka huu 2024. Iran imeibuka mshindi kwa kuzoa medali 5 za dhahabu na 2 za fedha. Aidha wanamieleka hao wa Kiirani wamezoa jumla ya alama 183, na kuitumulia mavumbi Kyrgyzstan na Kazakhstan zilizomaliza za pili na tatu, kwa pointi 156 na 151 kwa usanjari huo.

 

Vitara: Iran mshindi wa 2

Timu ya wanaume ya Saber ya Iran imeshika nafasi ya pili kwenye Mashindano ya Mabingwa wa Asia kwenye mchezo wa vitara, baaada ya kuilemea Korea Kusini. Timu hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu ilifika hatua hiyo baada ya kuzipeleka mchakamchaka India na Kazakhstan kwenye mashindano hayo yaliyofanyika Kuwait. Iran imetunukiwa medali ya fedha kama ilivyotuzwa katika duru iliyopita ya mashindano hayo.

 

Mashindano hayo ya Asian Fencing Championships yam waka huu yalifanyika baina ya Juni 21 na 27 huko, Kuwait City, mji mkuu wa Kuwait.

Kombe la Dunia; Iran yapata kundi jepesi

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepangwa kwenye Kundi B ya duru ya tatu ya mechi za Asia za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026. Droo ya mechi hizo za kibara ilichezeshwa Alkhamisi huko Kuala Lumpur, Malaysia. Timu hiyo ya kandanda ya Iran ipo katika kundi moja na Iraq, Jordan na Oman, huku Palestina na Kuwait zikimezea nafasi mbili za mwisho za tiketi za moja kwa moja kundini.

Timu ya taifa ya soka ya Iran

 

Mechi za awali za kindumbwendubwe hicho zitapigwa kuanzia Septemba 5 mwaka huu hadi Juni 10 mwakani, ambapo washindi wa kwanza na wa pili katika kila kundi watajikatia tiketi za kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika katika nchi za Mexico, Marekani na Canada mwaka 2026.

Soka Afrika; Kombe la COSAFA

Timu ya taifa ya soka ya Kenya siku ya Jumapili ilishuka dimbani kuvaana na Comoro katika michuano ya Kombe la COSAFA (Baraza la Vyama vya Kandanda Kusini mwa Afrika). Wangazija ambao awali walitoa sare ya bao 1-1 na Lesotho, waliutandaza mpira na kucheza mchezo wa kiutu uzima, na hatimaye wakaishia kuibamiza Harambee Stars mabao 2-0. Kenya iliyaanza mashindano hayo vizuri, baada ya kuidhalilisha Zambia na kuinyeshea mabao 2-0 yaliyofumwa wavuni na Austin Odhiambo na Patrick Otieno.  Aidha siku ya Jumapili, Zambia na Zimbabwe zilitoana jasho katika Uwanja wa Isaac Wolfson mjini Eastern Cape. Zimbabwe ilisajili ushindi wake wa 2 kwenye mechi hiyo ya Kundi B kwa kuitandika Zambia 2-0.  

Mchuano wa Namibia na Angola katika Uwanja wa Nelson Mandela uliishia kwa sare tasa. Kabla ya hapo, mwenyeji Afrika Kusini ililazimishwa sare tasa pia na jirani yake Botswana kwenye mashindano hayo ya kieneo siku ya Jumamosi katika Uwanja wa Isaac Wolfson. Jumanne hii, Kenya itatoana udhia na Zimbabwe huku vijana wa Ngazija wakigaragazana na Chipolopolo wa Zambia ambao ndio mabingwa watetezi.

Dondoo za Hapa na Pale

Mwenyeji Ujerumani imetinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa Ulaya (EURO 2024) baada ya kuibamiza Denmark mabao 2-0 katika dimba la Signal lduna Park jijini Dortmund. Jamal Musiala alifunga bao lake la tatu kwenye michuano hiyo katika dakika ya 68, baada ya Kai Havertz kuiweka kifua mbele Ujerumani kwa mkwaju wa penalti kunako dakika ya 53.

 

Mchezo mwingine wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Uropa 2024 uliwakutanisha mabingwa watetezi Italia dhidi ya Uswisi jijini Berlin. Uswisi imesogea mbele baada ya ushindi wa kishindo wa mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Olimpiki wa Berlin. Wakati huohuo, mabao ya Cameron Howieson, Jesse Randall na Max Mata yalitosha kuipa New Zealand ushindi wa kishindo dhidi ya Vanuatu, katika Uwanja wa Freshwater. Siku ya Jumapili, Uhispania ilivuna ushindi mwingine mnono baada ya kuigaragaza Georgia mabao 4-1, wakati ambapo Uingereza ilikuwa ikiilima Slovakia mabao 2-1.

Na klabu ya Yanga ya Tanzania imeibuka bingwa wa Kombe la Safari baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Safari Champions katika dimba la Benjamin Mkapa. Mabao ya Yanga yalifungwa na️ Omary Mfaume, sekunde chache baada ya kupulizwa kipyenga cha kuanza ngoma, Shekhan Ibrahim dakika ya 11, Prosper Moses Samwel dakika ya 44 na Hussein Ibrahim dakika ya 50.

……………….MWISHO…………..

 

Tags