Mar 27, 2024 11:55 UTC
  • Sekta ya mafuta ya Sudan Kusini yaathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan

Machafuko na ukosefu wa usalama vinaweza kushtadi huko Sudan Kusini baada ya moja ya mabomba yake makuu ya mafuta linaloelekea katika masoko ya kimataifa kupitia nchi jirani ya Sudan kuathirika mwezi uliopita. Haya ni kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya uchumi. Wamesema kuwa kusitishwa uzalishaji wa mafuta huko Sudan Kusini kunaweza kuchochea pakubwa ghasia na ukosefu wa usalama nchini humo.

Imeelezwa kuwa bomba la kusafirisha mafuta la Sudan Kusini kuelekea katika masoko ya kimataifa lilipasuka mapema mwezi Februari mwaka huu katika jimbo la White Nile na kusababisha Kampuni ya mafuta ya Petroli ya Dar kusimamisha shughuli za upakiaji mafuta. Kasoro hiyo ilitokea katika eneo linalodhibitiwa na wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ambao wanaendesha vita vya kuwania madaraka dhidi ya jeshi la Sudan.

Sekta ya mafuta Sudan Kusini yaathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan 

Timu ya wataalamu wa masuala ya ufundi wameshindwa kulifikia bomba hilo kwa ajili ya matengenezo kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya pande mbili huko Sudan; jambo ambalo limezidisha wasiwasi kwamba uchumi wa Sudan Kusini upo katika ukingo wa kuporomoka.

Alan Boswell Mtaalamu kutoka kundi kwa jina la South Sudan for International Crisis Group amesema kuwa bomba hilo lililopasuka lilikuwa likichangia theluthi mbili au robo tatu ya mapato ya mafuta. Sudan Kusini itakabiliwa na mzigo mkubwa wa fedha za bajeti iwapo bomba hilo litashindwa kuanza kazi.

Ripoti ya mwaka 2022 ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa mauzo ya mafuta huchangia takriban asilimia 90 ya mapato ya Sudan Kusini.

 

Tags