Mar 02, 2024 11:50 UTC
  • Sudan Kusini: Madola makubwa yanatumia vikwazo kubinya nchi zinazoendelea

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini amesema moja ya changamoto kuu zinazozikabili nchi maskini za ulimwengu wa tatu ni vikwazo vya madola makubwa duniani dhidi yazo.

James Pitia Morgan amesema hayo katika mkutano wa Jukwaa la Diplomasia la Antalya (ADF) na kuongeza kuwa, "Vikwazo vinatumiwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia na mataifa yenye nguvu kuziwekea mashinikizo nchi zinazoendelea."

Amesema nchi za Afrika zina ardhi pana, maliasili nyingi na rasilimali watu na kwamba, "Kitu pekee ambacho hatuna ni mtaji, kwa kuwa mtaji huo unadhibitiwa na nguvu ambazo hatuwezi kuzikaribia."

Amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, nchi za Magharibi zinafanya hima kuimarisha ubeberu wao kwa kutumia vikwazo kwa upande mmoja, na kuiba rasilimali za mataifa mengine hasa maskini kwa upande mwingine.

Wakati huo huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Guinea Bissau amesema nchi 33 kati ya 46 zinazokuwa duniani zinapatikana barani Afrika na kuongeza kuwa: Nchi hizi haziwezi kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya UN (SDSs) kufikia mwaka 2023 kutokana na ukosefu wa uadilifu duniani.

Carlos Pinto Pereira amewahutubu watawala wa Magharibi kwa kusema: Viongozi wa Magharibi wana maradhi na uchu wa kupora mali na rasilimali za wengine bila mipaka yoyote.

Naye Sylvie Baipo-Temon, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameeleza bayana kuwa: Tumeisha kama nchi koloni kwa muda mrefu, na hii leo tungali tunakabiliwa na ukoloni mambo-leo. Hili linatuzuia kujiwekea malengo ya uchumi wetu. Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, vikwazo vya Magharibi kinyume na matarajio yao, imekuwa chachu ya kupangua na kupanga upya siasa za dunia.

Tags